Bossou aomba kurudi kukipiga Yanga

Muktasari:

Hafidh kila Mwanayanga anatambua mchango wa Bossou katika misimu miwili aliyoitumikia timu yetu mimi ni kweli nina mawasiliano naye ya karibu na kila mara ananishawishi nizungumze na viongozi aweze kurudi.

Dar es Salaam. Wakati pazia la usajili likitarajiwa kufunguliwa la Alhamisi hii, beki wa kimataifa wa Togo, Vincent Bossou ameomba kurejea katika kikosi cha Yanga.

Bossou kwa sasa anaichezea klabu ya Saigon FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Vietnam, amefungua milango kwa Yanga kumsajili wakati litakapofunguliwa dirisha dogo Novemba 15.

Mratibu wa Yanga, Saleh Hafidh alisema amekuwa akiwasiliana mara kwa mara nyota huyo akiomba kurejeshwa katika kikosini katika dirisha dogo la usajili ili aendelee kuisaidia timu hiyo ambayo haina msaidizi wa Yondani.

"Bossou amekuwa akiniomba sana arudi, sasa kwa kuwa kocha hayupo namsubiri arudi ili nimueleze kama atakubali kwakuwa hata yeye alisema anahitaji kuongeza mchezaji katika nafasi hiyo," alisema Hafidh.

Kwa mujibu wa kocha Mkuu wa klabu hiyo, Mwingi Zahera alikiri kutafuta beki wa kati ambaye ataongeza nguvu kikosini kwake dirisha dogo la usajili linalotarajiwa kufunguliwa hivi karibuni.

Zahera alipotafutwa kwa ajili ya kuzungumzia hilo alisema kwa sasa yupo na majukumu ya timu yake ya taifa na kuombwa kutafuta baada ya kurejea nchini.

"Huku pia nipo kazini na nimeomba ruhusa kwa uongozi umenipa nafasi ya kuja kulitumikia taifa langu ishu za Yanga kwa sasa siwezi kuzipa kipaumbele kwa sababu nipo nje ya majukumu naomba unitafute nikirejea nchini ili niweze kulizungumzia zaidi," alisema Zahera.

Bossou aliichezea Yanga kwa mafanikio kwa misimu miwili mfululizo baada ya kumaliza mkataba wake alitimka nchini kutokana na Yanga kushindwa kufikia makubaliano naye.