Bosi Yanga amfutia kesi Haji Manara

Muktasari:

Cha kufurahisha zaidi, aliyetangaza kumfungulia ni Mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Abbas Tarimba, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya TFF.

SIMBA wana kila sababu ya kufurahia taarifa hii baada ya Msemaji wao, Haji Manara, aliyekuwa kifungoni sasa kufunguliwa na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF).

Cha kufurahisha zaidi, aliyetangaza kumfungulia ni Mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Abbas Tarimba, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya TFF.

Manara, mtoto wa nguli wa soka nchini, Sunday Manara, alijitia matatizoni na TFF na kufungiwa kujihusisha na soka kwa mwaka mmoja na faini ya Sh9 milioni, ila aliomba marejeo ya hukumu yake katika Kamati ya Nidhamu iliyomwachia huru.

Tarimba ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya SportPesa Tanzania, alisema uamuzi wa kumfungulia Manara na wenzake walioomba mapitio ya hukumu zao, unalinda maslahi ya soka la Tanzania.

Mbali na Manara, wengine waliofunguliwa ni Ayoub Nyaulingo, Blassy Kiondo na James Makwenya ambao walifungiwa kwa kosa la kukaidi maagizo ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF.

“Ilifika hatua watu walianza kutoleana maneno ya kashfa na dharau jambo ambalo halitoi picha nzuri kwa maendeleo ya soka, hivyo kamati iliona haja ya kufanya mapitio ya uamuzi uliotolewa kwa baadhi ya waliofungiwa,” alisema Tarimba.

“Kuna wengine ambao hawakupata nafasi ya kusikilizwa na kanuni zinatoa nafasi kwa kamati kufanya marejeo ili kuona kama kuna ushahidi ambao haujaangaliwa ambao ungeweza kufanya hayo mambo yasifike hapa tulipo.”

Manara amepokea msamaha huo kwa furaha akisema anamshukuru Mungu kwa kilichotokea na kuwashukuru akina Tarimba na wenzake kumuondolea adhabu hiyo.

“Sipendi kufukua makaburi, yatupasa sote tusonge mbele, hakuna aliyeshinda. Umeshinda mchezo wa soka. Naahidi kuendelea kufanya kazi kwa weledi na nidhamu,” alisema.