Boomplay yaupaisha muziki wa Bongo Fleva kimataifa

Muktasari:

Ushirikiano huu pia utawawezesha wasanii wa Warner Music kujitangaza zaidi na pia kwa haraka mbele ya mamilioni ya watumiaji wa Boomplay na kuiwezesha app hiyo  kuifikia dhamira yake ya kukusanya kazi za muziki kutoka sehemu mbali mbali za dunia na kuzileta barani Afrika.

MUZIKI wa Bongo Flava umezidi kutanuliwa baada ya Kampuni ya Boomplay kusaini makubaliano ya kibiashara na Warber Music kwa lengo la kuongeza wigo wa upatikanaji wa muziki wa kampuni hiyo maeneo mengi duniani.

Moja kati ya makubaliano hayo ni pamoja na kuipa fursa Boomplay, kusambaza kazi za muziki zaidi ya milioni moja kutoka Warner Music kwenda kwa watumiaji wake nchini Tanzania na mataifa mengine tisa ya kiafrika ikiwemo Cameroon, Ivory Coast, Ghana, Kenya, Nigeria, Rwanda, Senegal, Uganda na Zambia.

Ushirikiano huu pia utawawezesha wasanii wa Warner Music kujitangaza zaidi na pia kwa haraka mbele ya mamilioni ya watumiaji wa Boomplay na kuiwezesha app hiyo kuifikia dhamira yake ya kukusanya kazi za muziki kutoka sehemu mbalimbali za dunia na kuzileta barani Afrika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Boomplay, Bwana Joe He alisema, “Makubaliano haya na makampuni makubwa ya muziki ya kimataifa kama Warner Music, yanatuwezesha sisi kuyakaribia mafanikio ya malengo yetu ya kujenga jukwaa kubwa la muziki linaloaminika na wengi barani Afrika.”

“Tunataka kila mpenda muziki awe na uwezo wa kupata nyimbo na video, wakati wowote na mahali popote. Tunatarajia uwepo wa mafanikio bora kupitia ushirikiano huu na muendelezo mzuri wa kibiashara tukiwa na Warner Music hasa katika kipindi hiki kizuri kwenye fani ya muziki Afrika” aliongeza Bwana He.

Pia, Meneja wa Boomplay Tanzania, Bi Natasha Stambuli alisema, “Tunatarajia mafanikio makubwa na fursa mbalimbali yakiwa ni matokeo ya makubaliano kama haya katika tasnia ya muziki nchini Tanzania. Huu ni mwanzo wa mambo makubwa zaidi hapo mbeleni kwa Boomplay pamoja na Warner Music.”

Naye Alfonso Perez Soto, ambaye ni Makamu wa rais wa Warner Music huko Ulaya Mashariki, Mashariki ya Kati na Afrika amebainisha kwamba “Tuna furaha kushirikiana na Boomplay kuleta kazi kutoka kwa wasanii wetu kwa mamilioni ya wasikiliza na wapenzi wa muziki barani Afrika. Boomplay tayari imewafikia watu wengi barani Afrika huku wakiendelea kupanua wigo. Hii ni fursa kubwa kwa wasanii wetu kupata mashabiki wengi zaidi.”

Tangu mwaka jana, Boomplay imeendelea kutikisa anga la muziki kwa kutangaza ushirikiano na makampuni mbali mbali makubwa ili kupata watumiaji wengi zaidi kila mwezi na kutoa version (toleo) ya iOS mwezi Disemba mwaka 2018.

Pamoja na uwepo wa lebo kubwa za muziki zinazojiunga na Boomplay, app hii imejidhatiti kwa kujenga na kuboresha nafasi yake barani Afrika. Boomplay, ambayo mpaka kufikia mwezi Februari, 2019, ilijikusanyia zaidi ya watumiaji milioni 42, ina kazi za muziki zaidi ya nyimbo milioni 5, na maelfu ya video kutoka kwa wasanii wa Tanzania na wa kimataifa.