Bongo zozo : Mcheki Mzee wa Fujo Zisizoumiza

Muktasari:

Ukiiona sura yake, kisha ukasikia kiswahili anachoongea utapata shaka na kushtuka juu ya jamaa kumudu kutumia lugha hiyo pamoja na utani mwingi alionao na hicho ndicho kilichomfanya ajizolee umaarufu na kupendwa na kila shabiki aliyesikia au kumuona karibu yake.

WAKATI baadhi ya mashabiki wa soka wakiendelea kumjadili, Pierre Liquid kupelekwa Misri kuishangilia Timu ya Taifa, Taifa Stars mjini Cairo kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019, kuna jamaa aliyegeuka kivutio.

Jamaa huyo aliyekuwa kivutio kwa jinsi alivyokuwa akiishangilia Stars na kuonyesha mapenzi makubwa akisafiri kutoka Uingereza hadi Misri, sio mwingine ila ni raia wa Uingereza anayetambulika kwa majina ya Nick Reynolds maarufu kama Bongo Zozo a.k.a Mzee wa Fuzo Zisizoumiza.

Ukiiona sura yake, kisha ukasikia kiswahili anachoongea utapata shaka na kushtuka juu ya jamaa kumudu kutumia lugha hiyo pamoja na utani mwingi alionao na hicho ndicho kilichomfanya ajizolee umaarufu na kupendwa na kila shabiki aliyesikia au kumuona karibu yake.

Mzee wa Fujo Zisizoumiza ndio, ni msemo anaoupenda kuutumia kila anapopiga stori na jamaa aliokuwa akikutana nao katika viwanja na hata hoteli iliyokuwa inatumiwa na Taifa Stars pale Misri.

Msemo wa fujo zisizoumiza analenga, mtu anaweza kuwa na vurugu, lakini zisiwe na madhara kwa mtu wala vitu vyake akimaanisha kutaniana tu lakini huhatarishi amani.

Kwa umaarufu huo, Mwanaspoti likamtafuta Bongo Zozo na kutaka kujua mambo machache kuhusu historia yake ya maisha na juu ya kuipenda Tanzania.

KAZALIWA WAPI?

“Nimezaliwa Zimbabwe, lakini nilipokuwa mdogo wazazi wangu walienda Uingereza, nimekulia sehemu moja inayoitwa Norwich na timu yangu inaitwa Norwich City, tumepata bahati tunaingia Ligi Kuu msimu ujao,” anasema Bongo Zozo.

KAJUAJE KISWAHILI

“Nilivyokuwa na miaka 20 wakati nimemaliza chuo, nilipanga kuja Afrika na nikachagua Tanzania. Nilipanga kukaa miezi mitatu, ikawaje nikakaa miaka 18? Ni kwa sababu ya mwanamke, lazima niseme ukweli,” anasema na kuongeza:

“Nilimuona binti mzuri sana Mtanzania Carolina, nikaja kumuoa ni Mchaga mtoto mzuri sana, baba yake alikuwa Mwalimu wa Lugalo alikuwa anaitwa Mzee Matero ni marehemu sasa. Huyu ndiye aliyenifanya nikae muda mrefu na kukijua Kiswahili.”

Anafichua tangu amekuwa Tanzania na kupendana na mkewe wamefanya mambo makubwa anayojivunia, mbali na kujifunza Kiswahili kilichompa umaarufu mkubwa.

“Uhusiano wetu ukaanzia hapo na baadaye tukafanya kazi pamoja, nilifungua kampuni ya kufuga kuku kule Iringa, tulikuwa tunafuga kuku wa kienyeji tuliokuwa tunagawa vijijini, baada ya hapo nilienda Moshi nikaingia kwenye kazi ya kahawa.

Ilikuwaje akatoka Dar mpaka Iringa? Bongo Zozo anajibu: “Nilienda Iringa moja kwa moja nilivutiwa na baridi nikasema hapa nitaishi na ndiko nilikokutana na huyo binti ambaye kwa sasa ndiye mke wangu, alikuwa anaishi pale ndio nikaamua kuishi pale nilipata marafiki wengi kuliko popote.”

Alipoulizwa alipata ugumu wowote kumuoa Mtanzania? Naye anajibu:

“Ilikuwa rahisi sana, wanawake wa Kitanzania wana uvumilivu mkubwa sana, unajua wanaume tuna makosa mengi sana, kuna wakati tuliachana lakini akanisamehe kwa ajili ya kuhakikisha analea watoto wake vizuri.

“Uingereza mkiachana basi hakuna kuongea, tofauti na wanawake wa Kitanzania ambao wanavumilia vitu vingi, ila wanasuta ingawa mwisho wa siku wanasamehe.”

ETI AFRIKA KAMA ULAYA TU

Bongo Zozoz anasema haoni tofauti ya maisha ya Ulaya na Afrika na hajui kwanini watu hutamani sana kwenda Ulaya na kukimbia bara hili.

“Afrika kuna maisha bora nashangaa sana watu wanavyong’ang’ania Ulaya, ni kweli kuna vitu kama hospitali afya vinapatikana bure kule, barabara nzuri lakini vitu si utu, kule kila mtu kivyake hakuna muda wa mtu kwenda kwa mtu kama ilivyo huku,” anasema.

“Afrika kuna umoja sana kupitia michezo na mambo mbalimbali, mfano mtoto wangu wa kiume anaitwa Mickey (13) tulikuwa Moshi alikuwa anatoka shule nikamuuliza dada yake Jessica (16), Mick yuko wapi ananijibua anacheza mpira.

“Niliona hii ni hazina kwani Uingereza ukikuta watu wanacheza mpira njiani huwezi kuomba namba nami nicheze watakuona kichaa kabisa, lakini siku hizo mwanangu naenda kumtafuta nikakuta anarudi pekupeku ametoka kucheza mpira nilifurahi sana, unaona utu huo? Ulaya kule hakuna kitu kama hicho.”

“Mwanangu anapenda kuja kuwa mchezaji wa Taifa Stars, napenda namna anavyocheza kwa bidii akipata mchezo njiani anacheza, halafu Afrika wanacheza umri tofauti ndio maana hakuna uonezi sana, kule Uingereza ni wa umri wako tu.”

ASILI YA BONGO ZOZO

“Hili jina la Bongo Zozo maana yake ni fujo na wengi hawaamini, lakini hii ni lugha ya Kishona inayotumiwa kule Zimbabwe pamoja na Kindebele, ndio maana napenda kusema mimi ni Mzee wa Fujo zisizoumiza.”

JAMAA NI KOCHA BUANA!

Bongo Zozo anaelezea juu ya taaluma yake na kuweka bayana kuwa yeye ni kocha wa soka.

“Mimi ni kocha wa soka nina cheti kabisa cha taaluma hiyo, nafundisha watoto kila Ijumaa tulikuwa tunakutana kucheza mpira, tulikuwa na fujo zisizoumiza ni raha sana mnapokutana wakati wa mapumziko baada ya kazi ngumu unajua ni raha sana.”

“Nilikuwa na kina Muba, Ahmed Mohamed, ilikuwa raha sana kwani ni raha kukutana mwisho wa wiki kuondoa uchovu wa kazi za kila siku, tulifurahia kwa kweli,” anaongeza.

SASA ANAISHI WAPI?

“Kwa sasa naishi Uingereza ambako nafanya biashara zangu za mitandao ‘youtube’ ndizo ninazofanya.

“Ninaishi na mke na watoto wangu, nina binti yangu ana miaka 16, najivunia kuwa na watoto ambao ni Watanzania, hilo najivunia sana, watu wengi wakiniona ni shabiki mkereketwa wa Taifa Stars,” anasema na kuongeza:

“Kuna watu wakiniona ninavyoshabikia Tanzania wanatamani kunipa zawadi, ninachosema zawadi ya watoto wangu inatosha sana, nitakuwa nashabikia taifa hilo mpaka kufa kwangu.

“Afrika kama mtoto ameanguka wengine wanampa pole, ila Uingereza wanacheka, sasa watoto wangu ni Watanzania haswa hilo najivunia na kuipenda mpaka kufa licha ya mimi kuwa Muingereza.”

ANAKUJA TANZANIA?

“Ndio, nakuja mara kwa mara kuna chama changu cha gofu, tunajiita Wanyalukolo, nilikuja Tanzania nikiwa na miaka 21, ni kama Tanzania imenikuza, nilipokuwa Iringa nilikuwa na marafiki watano wote ni Waingereza na tumeoa Tanzania, maisha yetu yapo sawa, ingawa tumesambaratika.

“Kuna aliyepo Kenya, mwingine Dar es Salaam, wawili Uingereza huwa tunakutana mara moja kwa mwaka, hasa wakati wa Pasaka, tunakuwa tunaisubiri sana hiyo siku.”

ANAZUNGUMZA KISWAHILI KWAO?

“Sema najikaza, nikiona Mwafrika yeyote, Uingereza namuangalia namsalimia najua kabisa wanapenda, huwa nauliza wanatoka nchi gani, haijalishi iwe ametoka Ghana yaani popote pale nikimsalimia lazima nitaingiza Kiswahili kidogo.

Alipoulizwa lugha ipi kati ya Kiingereza na Kiswahili apendacho kuzungumza?

“Naona raha kuongea Kiswahili, huwa watu wananishangaa na kuamini nitakuwa nimefanya makubwa kwenye nchi hiyo lakini nimeipenda Tanzania kama ilivyo tu napenda ukarimu wa watu wa nchi hii.”

Je, unajua Bongo Zozo hapendi kuitwa Mzungu, unadhani kwanini? Endelea naye Alhamisi.