Bondia Mwakinyo awatikisa Matumla, Cheka

Muktasari:

  • Mwakinyo alianza kung'aa kwenye ngumi mwaka jana alipomchapa aliyekuwa bondia namba nane wa dunia, Muingereza Sam Eggington kwa Technical Knock Out (TKO) pambano lililoshtua Uingereza na kumpandisha Mtanzania huyo hadi kuwa bondia wa 19 na sasa ni wa 18 wa dunia

Dar es Salaam. Baada ya kupanda na kuwa bondia wa 18 wa dunia, Hassan Mwakinyo anaangaliwa kama mrithi wa nyota wa zamani wa ndondi, Rashid Matumla (Snake Man), Francis Cheka (SMG) na Mbwana Matumla (Golden Boy)

Mabondia hao wamewahi kuweka rekodi katika orodha ya mabondia bora wa dunia katika uzani tofauti, ambapo sasa Mwakinyo ndiye 'jicho' la ngumi la Tanzania dunia.

Matumla bingwa wa zamani wa dunia wa WBU enzi zake amewahi kuwa bondia wa 20 wa dunia, huku Mbwana ambaye ni mdogo wake akiwa wa saba na Cheka bingwa wa zamani wa dunia wa WBF akiingia kwenye 'top 30' ya dunia.

Kwa mujibu wa mtandao wa ngumi wa dunia (boxrec) Mwakinyo ambaye miezi kadhaa iliyopita aliporomoka na kuwa bondia wa 22 amepanda tena na sasa ni bondia wa 18 wa dunia kwenye uzani wa welter.

Akizungumzia rekodi hiyo ya Mwakinyo, Mbwana alisema ili aiendeleze bondia huyo hana budi kucheza mapambano na mabondia wenye rekodi nzuri.

"Mimi hadi nakuwa bondia wa saba nilipigana na kuwa bingwa wa dunia wa WBU, WBA na IBO," alisema Mbwana aliyekuwa akipigania uzani wa super fly.

Matumla alimshauri Mwakinyo acheze mapambano ya mara kwa mara vinginevyo atatolewa katika rekodi.

"Anapaswa kucheza na bondia mwenye rekodi nzuri, sio bondia wa 100 ambaye hata akishinda hamuongezei chochote katika kulinda rekodi yake, kwani hiyo ndiyo changamoto kwa bondia anapokuwa kwenye rekodi nzuri ya dunia," alisema.

Francis Cheka ambaye alishushwa kwenye rekodi na kuvuliwa ubingwa baada ya kufungwa jela, alisema rekodi ya Mwakinyo itazidi kupanda endapo atacheza mapambano na mabondia wa levo yake.