Bodi yafuta mechi za usiku, Simba na Yanga

Mechi za Simba na Yanga hasa zilizokuwa zifanyike kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku, sasa zote zitafanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Bodi ya Ligi imetangaza hivyo.

 

Tayari Yanga walishaanza kutumikia uamuzi huo baada ya mechi yao ya jana dhidi ya Polisi Tanzania iliyokuwa imepangwa kufanyika saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Mkapa kuchezwa saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Uhuru.

 

Mechi nyingi za Simba na Yanga zilipangwa kuanza saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Mkapa lakini sasa zote itabidi zichezwe saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Uhuru kutokana na uwanja huo kutokuwa na taa za uwanjani  mbazo zinakidhi mechi kuchezwa usiku.

 

Ukiondoa mechi ya  jana ya Yanga na Polisi Tanzania, mechi nyingine ambazo itabidi muda wake wa kufanyika ubadilishwe ni tatu zijazo za Simba ambazo ni dhidi ya  Ruvu Shooting utakaofanyika Jumatatu ijayo, dhidi ya Mwadui (Oktoba 31) na dhidi ya  Kagera Sugar utakaofanyika Novemba 4.

 

Yanga yenyewe mechi zote tatu zijazo itakuwa ugenini kuikabili KMC Jumapili kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza kisha itacheza na Biashara United Oktoba 31 kwenye Uwanja wa Karume Mara halafu itaumana na Gwambina Novemba 4 kwenye uwanja wa Gwambina Complex Shinyanga.

 

Taarifa ya Bodi ya Ligi imesema" Bodi ya Ligi Tanzania  inawataarifu kuwa mechi zote  za Ligi kuu Bara  msimu wa 2020/2021 zilizopangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa sasa zitachezwa kwenye Uwanja wa Uhuru hadi hapo uwanja utakapofunguliwa"

 

"Wakati huo huo mechi zote za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza zilizokuwa zichezwe kwenye uwanja wa  Jamhuri Dodoma sasa zitachezwa  kwenye uwanja wa Samora Iringa (kwa mechi za Ligi Kuu) na Jamhuri Morogoro (Daraja la Kwanza).

 

Katika msimu huu wa Ligi, Simba imecheza mechi mbili na Yanga imecheza mechi tatu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa zote zikichezwa kuanzia saa 1.00 usiku.

 

Yanga imevuna pointi saba katika mechi tatu ilizocheza ambapo ilitoka sare ya bao 1-1 na Prisons, ikaifunga Mbeya City kwa bao 1-0 na kisha ikaichapa Coastal Union kwa mabao 3-0.

 

Simba yenyewe imekusanya pointi sita katika mechi mbili ndani ya Dimba la Benjamin Mkapa ambapo ilishinda mabao 4-0 dhidi ya Biashara United na iliichapa Gwambina kwa mabao 3-0.