Bocco amtaja Kocha Simba

NAHODHA wa Simba, John Bocco amezungumza na mashabiki wa klabu hiyo na kuwapa ufafanuzi wa ishu mbalimbali zinazoendelea kwenye kikosi hicho huku akigusia ishu yao na Kocha Sven Vandebroeck.

Bocco ambaye alirejea uwanjani kwenye kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting akitokea kwenye majeraha, alizungumza na mashabiki hao kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram.

Katika ukurasa huo aliposti hali ilivyo ndani ya kikosi na kuwaomba radhi mashabiki ambao kwa nyakati tofauti alijibu maswali yao likiwemo la wao kuwa na ugomvi na Kocha Sven, ambapo alisema: “Hakuna kitu kama hicho.”

Bocco ambaye aliikosa pia mechi dhidi ya Prisons pale Simba walipofungwa bao 1-0 mjini Mbeya, aliwatuliza mashabiki kwa kuwaomba radhi kwa niaba ya wachezaji wenzake. “Tunarekebisha makosa yetu na kurudi kwenye sura mpya na upambanaji mpya kwa michezo yote ijayo ili turudishe furaha yetu, kwa kupata matokeo mazuri kama tulivyozoea, tumeshawaangusha tunakiri hili ila tunaamini hali hii haitajitokeza tena kwa michezo ijayo, nguvu moja,” aliandika Bocco ambaye ni mchezaji wa zamani wa Azam.

“Kama mnavyotusifia tukifanya vizuri, pia ni jukumu letu tukifanya vibaya zaidi kuheshimu maumivu yenu mashabiki, kukosea kupo na tutakosea tu ila haina maana kuwa ukikosea ushindwe kuwa muungwana.”

“Hii posti sio kama tunawaogopa nyie mashabiki au hatutafungwa tena, bali ni kuonyesha pia sisi tunajali na hatukupenda itokee ni kuwapa moyo tu mashabiki wetu kuwaonyesha sisi hatujakata tamaa na hatukati, tunapambana kwa ajili ya klabu yetu, ila sio kinyonge kama ulivyouliza wewe.” Katika mchezo huo, kiungo nyota Jonas Mkude alikuwa amevaa kitambaa cha unahodha, huku nahodha wa awali Mohamed Hussein akiwa uwanjani.

Mashabiki walishangaa hata pale alipoingia Bocco kuchukua nafasi ya Lary Bwalya, ambapo hakupewa kitambaa na Mkude na kuona kama vile ameshaporwa cheo hicho, lakini alipoulizwa na mashabiki alisema hakuna shida.

“Hapana mimi ni nahodha wa Simba mpaka leo hii, ila kilichotokea nilivyoingia (uwanjani) timu ilikuwa tayari nyuma kwa goli moja na sio Jonas wala mimi aliyewaza kunipa au mimi kuchukua kitambaa, akili zetu za kibinadamu zilikuwa ni kurudisha goli na kutafuta la ushindi, hicho ndicho kilichotokea, ila mimi ni Simba mpaka leo hii.”