Bocco aliamsha tena Simba

Muktasari:

Akisisitiza licha ya kutambua si kazi rahisi, kitu kinachompa moyo ni kuona wanaomiliki mabao mengi ni wachezaji kama yeye, wanafanya mazoezi kama yake, hivyo anachopaswa kukifanya ni bidii ili mwisho wa msimu aishi ndoto yake.

OLIPA ASSA

KAMA ulidhani nahodha wa Simba, John Bocco hayumo kwenye kinyanganyiro cha kiatu cha dhahabu kwa msimu huu utakuwa umechemka, hiki ndicho alichokisema baada ya kufunga bao mojawapo kati ya 3-0 timu hiyo ikicheza dhidi ya Mwadui FC juzi Alhamisi.

Bocco alisema kitendo cha kutikisa nyavu dhidi ya Mwadui, Simba ikishinda mabao 3-0, kimempa ari na nguvu ya kwenda kunoa upya mguu wake kwa madai anataka kuingia kwenye vita ya kuwania kiatu cha dhahabu dhidi ya wale wanaomiliki mabao mengi kama Heritier Makambo (Yanga), Said Dilunga (Ruvu), Meddie Kagere na Emmanuel Okwi (Simba).

Akisisitiza licha ya kutambua si kazi rahisi, kitu kinachompa moyo ni kuona wanaomiliki mabao mengi ni wachezaji kama yeye, wanafanya mazoezi kama yake, hivyo anachopaswa kukifanya ni bidii ili mwisho wa msimu aishi ndoto yake.

“Najipanga na kila kitu ni dhamira ya dhati, kwanza nianze na kuvunja rekodi yangu mwenyewe ya mabao 14 niliomaliza nayo msimu uliopita kisha niingia anga za kuwania kiatu cha dhahabu.

“Pamoja na kwamba natamani hilo, jambo la msingi zaidi ni kuhakikisha natimiza malengo ya klabu pale inapopatikana nafasi ya mwingine kufunga afanye hivyo, kikubwa ni timu ipate pointi tatu muhimu,” alisema.

Alipoulizwa viporo vinawapa changamoto gani! Bocco alijibu kuwa “Raha yake ni kushinda vyote, timu tunazokutana nazo zina ushindani wa hali ya juu mfano mzuri umeona namna ambavyo walikuwa wanacheza Mwadui FC.

“Tunahitaji kukomaa ili tuweze kuvimaliza kishujaa kwani timu tunazokutana nazo baadhi zimeanza kucheza mechi za mzunguko wa pili ambao unakuwa umebeba ndoto za klabu zipo zile zinazojikwamua na kushuja daraja, nyingine kuwania nafasi tatu za juu na zile za ubingwa.

“Mashabiki wasichoke waambatane pamoja na sisi kuhakikisha tunafikia kwa pamoja malengo yetu ya kutetea ubingwa hata sisi wachezaji tuongeze juhudi zaidi,” alisema.