Bocco, Wawa mtegoni

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi alipoulizwa kuhusu ishu ya mkataba wa Aussems na wachezaji wanaoelekea kumaliza mikataba yao Msimbazi alisema kila kitu kinaelekea pazuri kwani yote yamo ndani ya uongozi huo na hasa mkataba wa Aussems.

WAKATI mashabiki wa Simba wakianza kukisahau kipigo cha juzi Jumamosi ilichopata timu yao kutoka kwa Kagera Sugar, imebainika mabosi wa klabu hiyo wamemuachia kazi Kocha Mkuu wao, Patrick Aussems kuamua hatma ya nyota 10 wa kikosi hicho kubaki Msimbazi kwa msimu ujao.

Inaelezwa kuwa mabosi wa Simba ambao wanaendelea kuvutana juu ya hatma ya mkataba mpya wa kocha huyo Mbelgiji, wamemtaka Aussems kupeleka orodha ya majina ya wachezaji ambao mikataba yao inamalizika iwapo kama bado wanahitajika kwa msimu ujao.

Katika kikosi hicho cha Simba wachezaji ambao wanamaliza mikataba yao ni nahodha John Bocco, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Aishi Manula, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, James Kotei, Pascal Wawa, Asante Kwasi na Nicholas Gyan.

Ukimuondoa Kapombe ambaye ni majeruhi, waliosalia baadhi yao wapo kwenye kikosi cha kwanza na wamekuwa msaada mkubwa msimu huu katika Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika ambako Simba ilifika hatua ya robo fainali na kung’olewa na TP Mazembe ya DR Congo.

Kutokana na hali hiyo, nyota hao wa Simba ni kama wamewekwa mtegoni kwa kuhakikisha mechi zilizosalia za msimu huu wajitoe na kupambana kiume ili kuhakikisha wanamfurahisha Mbelgiji ili wabakishwe Msimbazi.

Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi alipoulizwa kuhusu ishu ya mkataba wa Aussems nawachezajiwanaoelekea kumaliza mikataba yao Msimbazi alisema kila kitu kinaelekea pazuri kwani yote yamo ndani ya uongozi huo na hasa mkataba wa Aussems.

“Tunafahamu kuna zaidi ya wachezaji saba ambao mikataba yao mwishoni mwa msimu huu lakini hakuna mchezaji atakayeachwa kwani mpaka sasa tunasubiri Aussems atoe mapendekezo yake kwa anaotaka wasaini mikataba mipya,” alisema Mkwabi

“Hata wachezaji wapya ambao tutawasajili msimu huu kuongeza nguvu katika timu yetu hakuna atakayesajiliwa bila idhini ya Aussems. Nguvu yetu kubwa ipo katika kuiweka timu kwenye mazingira mazuri wakati huu ili kuweza kufikia malengo ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara,” alisema Mkwabi.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori alisema kuhusu suala la kumpa mkataba mpya Aussems hilo lipo chini ya Bodi ya Wakurugenzi na muda utakapofika wataliweka wazi kama walivyofanya kipindi wanamuajiri.

Kuhusu ishu yausajili wa wachezaji, alisema suala la kumalizika kwa mikataba ya wachezaji wao saba kwao halina shida na hawana presha kwani wanasubiri kocha wao Aussems awapatie majina ya wale anaowahitaji waongezewe mikataba na wapya ambao atawapendekeza wasajili kwa ajili ya msimu ujao.

“Masuala yote ya usajili SImba mwenye kauli ya mwisho ni kocha, ndiyo maana Kapombe alivyoumia alipendekeza tumsajili Zana Coulibaly, hivyo hata katika kipindi hiki tutafanya vile ambavyo atataka katika masula yote ya usajili.

“Kwa maana hiyo wachezaji wote wanaomaliza mikataba hata Kapombe ambaye bado ni majeruhi wote wapo katika mipango ya Aussems kwani mpaka wakati huu hajapendekeza mchezaji wa kuachwa, wote tunaweza kuwapa mikataba mipya,” alisema Magori.

Kocha wa zamani wa Yanga, Kenny Mwaisabula alisema jinsi kikosi cha Simba kilivyokuwa msimu huu na hao wachezaji ambao wanamaliza mikataba wengi wao wametumika katika kikosi cha kwanza katika mshindano yote kwahiyo kumuacha mchezaji kama huyo ni kosa kubwa mno.

Mwaisabula alisema Simba msimu ujao wanatakiwa kupambana zaidi katika mashindano ya kimataifa kama watachukua ubingwa msimu huu, kwa maana hiyo wanatakiwa kuwa na wachezaji wazoefu na waliokaa kwa pamoja zaidi ya misimu miwili kwahiyo kama wakiachana na hao watakuwa wanaanza tena upya kutengeneza timu yao.

“Masuala yote ya kiufundi na usajili kwa ujumla yanatakiwa kuwa chini ya kocha wao Aussems na kwa akili ya kawaida sidhani kama kati ya hao wachezaji kuna ambaye atapendekezwa aondeke bali atatamani waongezwe mikataba mipya na kuendelea kubaki nao msimu ujao.

“Naona masuala ya usajili hapa kama bado viongozi hawajayaelewa kwani wachezaji muhimu kama hawa katika kikosi hawakutakiwa kuelekea mwisho wa msimu huku mikataba yao ikiwa ndio inamalizika ilibidi wapewe mikataba mipya mapema,” alisema.