Bocco, Kagere kimenuka Simba

Muktasari:

  • Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems ana mpango wa kuwatenganisha washambuliaji watatu wa kikosi chake, John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi katika uchezaji kwa sababu tangu aanze kufanya hivyo hajapata matokeo mazuri.

LICHA ya ushindi wa mabao 2-1 iliyopata Simba dhidi ya African Lyon, Kocha Mkuu wa timu hiyo Patrick Aussems amegeuka mbogo akikasirishwa na sakata la wachezaji wake walioitwa Taifa Stars, huku akiamua kuwatenganisha kikosini mastraika wake watatu.

Kocha huyo amefichua kuwa inawezekana ikawa vigumu kwa mashabiki wa timu hiyo kuwaona tena Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na nahodha John Bocco wakicheza pamoja kuanzia sasa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Aussems alisema kwa sasa ni vigumu kuanza kwa pamoja kwa washambuliaji wake hao kutokana na kutopata kitu anachokitaka tangu alipoanza kuwatumia katika mechi kadhaa.

Kocha huyo kutoka Ubelgiji, alifafanua kuwa, bado hajaridhishwa na matokeo ya nyota hao wanapocheza pamoja ambapo anafikiria kuwatenganisha ili kila mmoja kivyake kwa nia ya kuifanya timu ipate matokeo mazuri zaidi.

Alisema, hata kama Bocco anayemaliza adhabu yake kutumikia kadi nyekundu atarudi hatampanga na wenzake wawili na badala yake atakuwa akiwatumia wawili miongoni mwao na mmoja kusubiri benchi.

“Sijapata ninachokitaka wanapoanza wote watatu naona bado kuna shida nafikiri hatutawatumia wote kwa pamoja tunaweza kuanza na wawili kati yao.

Nawaamini washambuliaji wangu ninachofurahi nina nafasi kubwa ya kuchagua nani acheze na nani asubiri lakini jambo zuri zaidi wote wanafanya vizuri,” alisema Aussems.

Kagere, Bocco na Okwi wakitumika wawili kwa kupokezana wametengeneza mabao saba kati ya nane iliyonayo, Kagere alifunga manne, Bocco mawili na Okwi juzi alifunga moja. Bao jingine la Simba limefuingwa na winga, Shiza Kichuya na kuifanya Simba yenye washambuliaji zaidi ya sita kufunga mabao nane kwa wachezaji wanne tu.

STARS YAMCHEFUA

Kocha Aussems amewafuatilia wachezaji wake watatu ambao waliruhusiwa juzi ikiwa ni siku moja kabla ya timu yake haijacheza dhidi ya African Lyon kisha akasema hilo limemkera.

Kocha huyo ameungana na mwenzake wa Yanga, Mwinyi Zahera akisema kuchelewa kwa kujiunga kwa wachezaji wake katika kambi yao kimewaumiza wachezaji hao na kuwasababisha kuumia kirahisi.

Alisema ratiba ya mazoezi ambayo wachezaji wake watatu walikuwa wakipata Stars kiungo Jonas Mkude, Kipa Aishi Manula na beki Shomari Kapombe ni mara mbili kwa siku ambayo iliwapa urahisi kuumia katika mechi yao ya juzi.