Bocco, Kagere, wapewa bao 45

Muktasari:

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema kama washambuliaji wake watatu John Bocco,Meddie Kagere na Emmanuel Okwi wakitulia wanaweza kufunga mabao mengi msimu huu.
Aussems amesema washambuliaji wake hao wanaweza kufunga mabao kuanzia 10-15 kwa msimu kama wakipunguza kucheza kwa presha ya kunfa mabao.
Amesema tayari ameanza kulifanyia kazi kulifanyia kazi hilo kwa kuhakikisha washmabuliaji wake wanatulia katika kutumia nafasi wanazotengeneza katika mechi zao.

ACHANA na matokeo ya mechi yao ya usiku wa jana kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya African Lyon, Kocha Patrick Aussems amewaka kazi mastraika, Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na John Bocco kufunga jumla ya mabao 45 katika msimu huu wa Ligi Kuu. Kocha Aussems ambaye anakiri kwamba timu yake ilinyimwa bao halali lililofungwa na Okwi walipoumana na Yanga wikiendi iliyopita alisema, nyota wake hao kama wataamua kutulia Simba inaweza kuvuna mabao 45 kwa msimu mmoja.

Akizungumza na Mwanaspoti, Aussems alisema anatambua kwamba kikosi chake kina safu bora ya ushambuliaji ila nyota wao watatu akiwamo nahodha Bocco wanatakiwa kutuliza presha ili watupie mabao mengi. Raia huyo wa Ubelgiji alisema washambuliaji wake hao wamekuwa wakipata nafasi kubwa ya kucheza kama wakitulia kila mmoja anaweza kufunga mabao kati ya 10- 15 kwa msimu na hivyo kuibeba timu hiyo katika mbio za kutetea taji lao.

Alisema shida kubwa iliyopo kwa sasa ni washambuliaji hao kucheza kwa presha kubwa kuhakikisha wanafunga kitu ambacho kimekuwa kikiwafanya kupoteza nafasi nyingi na tayari ameanza kulifanyia kazi.

“Tuna safu bora ya ushambuliaji nina furaha na wachezaji wangu kama wakutulia naamini tunaweza kuwa na matokeo mazuri zaidi huko mbele,” alisema Aussems. “Sijawapangia washambuliaji wangu ni idadi gani ya mabao wanatakiwa wafunge kwa msimu, ila kwa hawa Bocco, Okwi na Kagere wanaopata nafasi mara kwa mara wanaweza kufunga kuanzia mabao 10-15 kwa msimu mmoja kila mmoja. “Tunatengeneza nafasi nyingi uwanjani tatizo ni utulivu katika kuzitumia, nilichogundua wanakuwa na presha ya kutaka kufunga nimeanza kulifanyia kazi hilo wanatakiwa kutulia mabao yanakuja tu.”

Kabla ya mchezo wa jana, Simba ilikuwa imefunga mabao sita tu, manne yakiwekwa kimiani na Kagere, huku mawili yakifungwa na Bocco ambaye alikuwa akitumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa kwenye mchezo wao dhidi ya Mwadui na kushinda mabao 3-1 kwa kosa la kumpiga ngumi beki Revocatus Mgunga.

BAO LA OKWI LAMLIZA

Kocha Aussems aliyeanza kuinoa timu hiyo tangu Julai mwaka huu, aliizungumzia mechi yao iliyopita dhidi ya Yanga na kudai ameona wachezaji wake wanaandamwa na kelele juu ya kuwaumiza wenzao wa Yanga, ila ameshafunga mjadala kwa kuwa hata wao walinyimwa bao halali. Aussems alisema anashangazwa kuona watu wanaongea sana juu ya makosa ya nyota wake, lakini wakishindwa kuongelea bao la Okwi la dakika 28 lililokataliwa.

“Sioni kama ni sahihi kwangu kuendelea na mjadala juu ya mechi ya Yanga naona watu wanaongelea sana juu ya suala la wachezaji wangu wanasahau ile mechi ilikuwa kubwa na ngumu,” alisema Aussems.

“Angalia mbona sioni watu wakiongelea bao ambalo tulilipata kipindi cha kwanza ambalo waamuzi walilikataa wakidai kulikuwa na kuotea hebu wakaangalie waone Simba ilivyonyimwa bao halali,” alihoji kocha huyo ambaye jana ulikuwa mchezo wake wa saba katika ligi, huku awali alishinda mechi tatu na kutoka sare michezo miwili na kupoteza moja dhidi ya Mbao FC ambayo usiku wa leo inavaana na Yanga Uwanja wa Taifa.