Bobby Williamson azikaba koo FKF, Gor Mahia

Muktasari:

  • Bobby anaiandama Klabu ya Gor, anayoidai nusu milioni, fedha anayosema ilistahili kuwa malipo ya bonasi yake kwa kuiongoza kutwaa ubingwa wake wa kwanza wa Ligi Kuu baada ya kulikosa kwa kipindi cha miaka 18.

Nairobi. KOCHA wa zamani wa Harambee Stars na klabu ya Gor Mahia, Mskochi Bobby Williamson ambaye kwa sasa anaumwa kansa, amesema hatachoka kudai kiasi kikubwa cha fedha anazodai kutoka kwa timu hizo mbili.

 Kocha huyo alisema anapanga kuzishtaki timu hizo mbili kwa Shirikisho la Soka duniani (FIFA) ikiwa zinaendelea kumkaushia.

Mskochi huyo alisema bado hajapokea Sh55 milioni anazolidai Shirikisho la soka nchini (FKF), kama fidia ya kumtimua kazi kwa kumvunjia mkataba kinyume cha utaratibu.

Lakini pia, Bobby anaiandama Klabu ya Gor, anayoidai nusu milioni, fedha anayosema ilistahili kuwa malipo ya bonasi yake kwa kuiongoza kutwaa ubingwa wake wa kwanza wa Ligi Kuu baada ya kulikosa kwa kipindi cha miaka 18.

Bobby ndiye aliyefanikiwa kurejesha ubabe wa Gor kwa kushinda taji hilo mwaka 2013 kwa mara ya kwanza baada ya kulikosa kosa kwa miaka yote hiyo.

“Nilitegemea mabosi wa shirikisho wangenitafuta tulijadili suala hili la marupurupu yangu, lakini baada yao kunilenga ndipo niliamua kupeleka ishu kwa Kamati ya Mizozo ya Kimichezo. Na ikiwa sitafanikiwa kupata uamuzi mwafaka basi, sasa nitaisogeza ishu mbele zaidi hadi kwa FIFA,” Williamson alisema.

 Kwa upande wa FKF, Shirikisho limesema kwamba linajitahidi sana kutafuta namna ya kumalizana na Williamson kwa sababu wakati wa kandarasi yake, maafisa waliopo kwa sasa hawakuwa ofisini wakati huo.

“Tulipopingia afisini tulirithi madeni kibao, ikiwamo yake Williamson. Katupeleka kortini na wala hamna kingine tunachoweza kufanya zaidi ya kusubiri uamuzi,” alisema afisa mawasiliano wa FKF, Barry Otieno.

Williamson alipigwa kalamu mara tu Rais wa sasa wa FKF, Nick Mwendwa, alipoingia afisini.

Nafasi yake ilipewa Kocha Stanely Okumbi aliyekuwa akilipwa Sh500, 000 kwa mwezi ikilinganishwa na Sh2.5 milioni alizokuwa akipokea Williamson.