Boban na Makambo mbona wasubiri tu

Muktasari:

  • Watu wengi wanasahau kwamba mchezaji huyu alikuwa katika kikosi cha African Lyon, huku akiwa mmoja ya wachezaji wenye msaada wa juu katika kikosi hicho.

Dar es Salaam. Usajili wa Haruna Moshi ‘Boban’ kutua Yanga umegusa hisia za watu wengi kiasi cha kuanza kuhoji umri wake na nafasi anayocheza.


Watu wengi wanasahau kwamba mchezaji huyu alikuwa katika kikosi cha African Lyon, huku akiwa mmoja ya wachezaji wenye msaada wa juu katika kikosi hicho.
Tuangalia namna ambavyo Boban amekuwa akicheza, limeona baadhi ya vitu ambavyo anavyo na akivichanganya pamoja na Herieter Makambo atakuwa na msaada mkubwa katika kikosi cha Yanga.


KONTROO KAMA YOTE
Makambo sio mtu ambaye anaweza kumiliki mpira kwa muda mwingi, mara nyingi amekuwa ni mchezaji ambaye anataka kutengenezewa na yeye kuweka wavuni.
Ujio wa Boban katika kikosi cha Yanga, kutaifanya safu ya ushambuliaji kuzidi kutulia kutokana na mchezaji huyo ana utulivu mwingi miguuni mwake.
Boban ana uwezo wa kuchezea mpira kwa muda mrefu na kukaa nao kisha akaanzisha mashambulizi kwa pacha yake ambaye atakuwepo katika eneo la ushambuliaji.


UTULIVU
Boban anapokuwa yupo uwanjani jambo la kwanza amekuwa nalo ni utulivu, sio mtu mwenye papara pindi anapokuwa yupo na mpira mguuni mwake.
Katika safu ya ushambuliaji kweny kikosi cha Yanga, amekosekana mtu ambaye anaweza kuweka utulivu na kupanga mashambulizi na Makambo, kwahiyo kuongezeka kwa Boban ni jambo la kheri.
Makambo ni mtu ambaye anahitaji kutengenezewa nay eye kuwa na kazi nyepesi ya kuweka tu wavuni, amekuwa akionekana katika mechi nyingi magoli anayofunga ni yale ambayo ametafuniwa kwa asilimia kubwa.


UKONGWE
Hakuna kijiji ambacho kinakosa mkongwe na ndio maana Yanga walifikia uamuzi ya kumsajili ili kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji katika kikosi hiko.
Licha ya kwamba amecheza soka kwa muda mrefu, Yanga wameangalia kwa jicho pana na kugundua kwamba mkongwe Mrisho Ngassa amekuwa na msaada katika kikosi chao hivyo wakavutiwa pia na huduma ya Boban licha ya kujua kwamba ni mkongwe.
Wanaamini kabisa kwamba Boban anamsaada mkubwa katika kikosi cha Yanga, kwani kutokana na ukongwe wake atamsaiidia Makambo kuweza kufanya vizuri katika mashindano ambayo wanashiriki.


MBINU
Boban amepitia katika mikono ya makocha wengi ndani na nje ya nchi ambao wamemfundisha kiungo huyu ambaye amekuwa hana maneno mengi anapokuwa yupo uwanjani.
Kwa kutumia uzoefu wake katika mbinu ambazo amebarikiwa kuwa nazo kiasi cha kutumia akiwa na African Lyon na kuisadia, mbinu hizo akizishusha katika kikosi cha Jangwani na kuchanganya zile za Zahera, bila shaka yeye na Makambo watakuwa moto wa kuotea mbali.