Bizimungu angalau sasa anapumua

Muktasari:

  • Kocha huyo pia alimpongeza straika wake, Salim Aiyee aliyetupia bao lake la 15 katika Ligi Kuu na kuzidi kuwafunika nyota wa kimataifa wa klabu kubwa za Simba, Yanga na Azam FC.

MWANZA.USHINDI wa mabao 3-1 iliyopata Mwadui FC juzi Jumapili dhidi ya Mbeya City katika mechi ya Ligi Kuu Bara umemfanya Kocha Ally Bizimungu kupumua akianza kusahau kipigo cha mabao 6-2 alichopewa na Ruvu Shooting wiki iliyopita mjini Mlandizi, Pwani.

Ushindi huo wa juzi umeifanya timu hiyo kufikisha pointi 36 na kukaa nafasi ya nane na kumfanya Kocha Bizimungu kusema wazi umemrejeshea matumaini na nguvu mpya ya kuzidi kukomaa kwenye ligi inayoongozwa na Yanga yenye alama 67.

“Mechi iliyopita tulipoteza ugenini na kutukatisha tamaa, kwani hatujawahi kukumbana na kipigo kikubwa kama kile, lakini angalau leo tumeshinda na niwapongeze wachezaji wangu kwa kubadilika kiasi cha kupata matokeo mazuri, niseme huu ushindi umerejesha nguvu mpya,” alisema Bizimungu.

Kocha huyo pia alimpongeza straika wake, Salim Aiyee aliyetupia bao lake la 15 katika Ligi Kuu na kuzidi kuwafunika nyota wa kimataifa wa klabu kubwa za Simba, Yanga na Azam FC.

Alisema siri ya mafanikio kwake ni kujituma na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi na kwamba iwapo ataendeleza kasi hiyo, basi Meddie Kagere (Simba) na Heritier Makambo wa Yanga watazidi kuisoma namba.

“Kwa ujumla Aiyee anajituma na anafuata maelekezo ya benchi la ufundi, kwahiyo kama ataendelea hivi, basi kina Kagere na Makambo wataendelea kuisoma namba katika mbio za ufungaji mabao,” alisema Bizimungu.