Bingwa wa dunia riadha awatupia dongo IAAF

Wednesday April 24 2019

 

BINGWA mara tatu wa dunia mbio za mita 1,500 Asbel Kiprop kaitupia dongo Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) baada ya kumpiga marufuku ya miaka minne kwa kosa la pufya.

Kiprop ambaye pia ni bingwa wa zamani wa Olimpiki, alifungiwa kushiriki riadha kwa kipindi chote hicho Jumamosi iliyopita na kitengo cha IAAF kinachoshughulikia Uwajibikaji wa Wanariadha (Athletics Interfrity Unit-AIU).

Vipimo vilivyochukuliwa Novemba 2017, vilipatikana  kuwa na chembechembe za dawa ya kusisimua misuli aina ya EPO.

Hata hivyo Kiprop ameendelea kusisitiza kuwa ni msafi huku akidai kuwa sio wafungwa wote walioko jela, walikosea.

“Ninachojua ni kwamba katika dunia hii hamna haki. Sio kila aliyetupwa jela ana hatia. Nitashauriana na wakili wangu kuhusu uwezekano wa kukataa rufaa dhidi ya uamuzi huu katika Mahakama ya Kimataifa ya Kimichezo (Court of Arbitration of Sport) kasema Kiprop mwenye miaka 29.

Staa huyo ameendelea kusisitiza kuwa, hakutumia EPO na hata ikiwa atalazimika kutumikia kifungo, chake haina noma bado tu atarejea kwa kishindo.

“Nasisitiza sikutumia pufya na nitaendelea kusisitiza hicho. Na hata ikiwa basi sitashiriki riadha kwa miaka minne, ipo siku nitarejea kwa kishindo,” aliongeza.

Kufuatia  hatua  hiyo, ushindi wake wowote wa kati ya Novemba 27, 2017 hadi Februari 3, 2018 umefutiliwa mbali.

Marufuku hiyo itamalizika Februari 2022 ikiwa tayari imerudishwa nyuma  na kuanzia Februari 2018 kuendelea.

Advertisement