Bilo mipango yaanza kunyooka Alliance

Muktasari:

Timu zinaendelea kujifua kujiandaa na msimu mpya wa ligi kuu Bara, kama ilivyo kwa Alliance inayojipima ubavu na mechi mbalimbali za kirafiki kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
 

KOCHA wa Alliance, Athuman Bilali 'Bilo' ameanza kutengeneza kikosi chake cha kwanza kupitia mechi za kirafiki ambazo kikosi hicho kinacheza kujiandaa na msimu ujao wa ligi kuu Bara.
Bilo amesema wamecheza na Tanzania Prisons walioifunga bao 2-0, Uwanja wa Nyamagana uliopo Mwanza, huku straika mpya wa timu hiyo, Jerry Tegete akiwa ametupia moja.
Amekiri kwamba ameanza kuona kombinesheni ya wachezaji kwa maana ya nani acheze na nani, akidai hilo linampa urahisi wa kutengeneza kikosi cha kwanza atakachofanya nacho kazi msimu ujao.
"Tunaendelea kucheza mechi mbalimbali za kirafiki na tayari tumecheza na Prisons, inanipa picha kamili ya kikosi cha kwanza lakini pia sabu makini, naamini msimu ujao utakuwa wa aina yake kwetu," amesema Kocha huyo aliyekuwa Stand United.
Bilo amesema wanatarajia kucheza na timu ya Rhaino na Pamba ya Mwanza, huku wakiendelea kusaka mechi nyingine zitakazowapima kikamilifu kabla ya kuanza kwa msimu.
"Nahitaji mechi nyingi zitakazonisaidia kukiweka sawa kikosi changu, msimu ujao utakuwa na ushindani mkali kujiandaa ni muhimu, timu zimesajili vizuri hivyo lazima kujiweka sawa," amesema.