Bilionea Yanga amjibu MO kitemi

Muktasari:

Tayari Yanga na GSM Foam, wamesaini mkataba huo na kwa sasa sasa jezi za Yanga nazo zitakuwa kama zile za watani wao, ukiacha jina la mchezaji mgongoni pia litakuwa na chata la GSM Foam na kuzidi kuineemesha klabu hiyo kifedha.

MASHABIKI wa soka wamekuwa wakichonga sana dhidi ya Yanga kutokana na bilionea wao, Mohammed ‘MO’ Dewji kumwaga mzigo wa maana Msimbazi na kelele zilizidi baada ya kuzindua jezi mpya zenye chata ya Mo Halisi juu mgongoni.

Mashabiki hao wamedai namna jezi za Simba zinavyoanza kuchafuka ni dalili njema ya kufuata mkumbo wa klabu kubwa Afrika na Duniani kuwa na machata yanayowaingizia fedha na hivyo ishu za kutembeza bakuli kama watani zao haitakuwapo.

Lakini sasa unaambiwa kilichofanywa na bilionea aliyeamua kumwaga fedha Jangwani kupitia udhamini wa jezi, ni kama vile amemjibu MO Dewji kibabe baada ya kutangaza mkwanja mwingine wa maana kupitia bidhaa zinazozalishwa na kampuni yake ya GSM.

Si mnajua kampuni hii inamilikiwa kigogo mmoja mwenye fedha zake za maana, Ghalib Said Mohammed, ambapo kampuni yake ndiyo inayosambaza jezi za Yanga msimu huu baada ya kuingia nao mkataba mnono ambao hata hivyo thamani yake haitajwi.

Sasa wakati hata mkataba wa mwanzo haujakauka wino, bilionea huo ameamua kumwaga mamilioni Jangwani kwa kuingia mkiataba wa mwaka mmoja wa kuidhamini Yanga kupitia magodoro yanayozalishwa na kampuni hiyo ya GSM ambayo chata lake litakaa mgongoni.

Tayari Yanga na GSM Foam, wamesaini mkataba huo na kwa sasa sasa jezi za Yanga nazo zitakuwa kama zile za watani wao, ukiacha jina la mchezaji mgongoni pia litakuwa na chata la GSM Foam na kuzidi kuineemesha klabu hiyo kifedha.

Mkataba huo ni mbali na ule ambao Yanga imekluwa ikionja fedha zake kuanzia kampuni ya Taifa Gas, Sportpesa ambao ni wadhamini wakuu, Maji ya Afya.

Meneja Masoko wa GSM, Hersi Said ameliambia Mwanaspoti katika mahojiano maalumu kwamba mzigo mpya wa jezi utaingia Septemba kwa njia ya bahari ambapo kila shabiki nchi nzima atapata jezi hizo zinazouzwa Sh 35,000.

Said alisema makubaliano ya mkataba huo na Yanga ni wa mwaka mmoja na ni wa fedha ambapo kiasi ni siri yao kwa mujibu wa mkataba waliosaini.

“Tuliomba kuwa wasambazaji na wauzaji wa jezi mpya za Yanga baada ya klabu kutangaza tenda. Tulishinda tenda hiyo, japo hatukuwa peke yetu, walikuwepo wengine walioomba ila vigezo vyetu vilitupitisha,” alisema na kuongeza;

“Sasa hivi tumeingia kama wadhamini kwa bidhaa nyingine ya magodoro, udhamini huu ni wa mwaka mmoja na ni wa pesa ambayo pande zote mbili umekubaliana, kwenye udhamini huu nembo yetu itakaa mgongoni juu ya namba ya mchezaji.”

“Hizi jezi zitakazokuwa na nembo ya GSM Foam zitaingia mwezi ujao na unakuja mzigo mkubwa unaopitia usafiri wa majini ambao ni wa bei nafuu ukilinganisha na kusafirisha kwa njia ya anga ambapo mzigo wenye kilo 30 unagharibu zaidi ya Dola 170,” alisema.

Kuhusu jezi, Meneja huyo alisema mzigo wa kwanza ulioingia ulikuwa mdogo kulinganisha na muda ambao waliingia mkataba huo.

“Ulikuwa muda mfupi sana tangu tuingie mkataba wa kuuza na kusambaza jezi za Yanga. Ikumbukwe ilikuwa ni katikati ya Julai na siku ya kilele cha Wiki ya Wananchi ilikuwa ni Agosti 4, jezi zilizinduliwa Agosti 2.

“Tulipata changamoto kubwa sana na ndipo tulipogundua Yanga ina mashabiki wengi na uhitaji ni mkubwa hivyo mzigo wa sasa ni mkubwa na utatosha nchi nzima, jezi zilizobaki sasa zinapatikana katika baadhi ya maduka yetu,” alisema

Alisema kila jezi inayouzwa Yanga wana asilimia yao ambayo hakutaka kuiweka wazi kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba wao.

“China kuna jezi nyingi unazikuta zimetengenezwa, lakini nyingine hazina ubora hivyo ilikuwa ni lazima tuwe na chaguo letu na kwa vile muda ulikuwa mdogo tuliona zitangulie baadhi kwa ajili ya uzinduzi na siku ya kilele cha Wiki ya Wananchi.

“Mkataba huu wa sasa ni wa mwaka mmoja huko mbele ukimalizika tutaangalia, maana tuliamua kuingia kwenye michezo hasa usambazaji wa jezi kwani kampuni yetu

inajihusisha zaidi na mavazi, hivyo tunaijua vizuri biashara hii” alisema Said

JEZI KWA VIGEZO

Ili kudhibiti uuzwaji kiholela pamoja na jezi feki, GSM inatarajia kutangaza nafasi kwa mawakala ambao watapitishwa kwa kuangalia vigezo vya kibiashara.

“Tutakuwa na mawakala nchi nzima ambao tutajiridhisha kama kweli ni mawakala halali kwa vigezo ambavyo tutaweka ikiwemo kuangalia TIN namba ya biashara, barua ya maombi, leseni ya biashara, eneo na picha ya biashara na cheti cha kampuni.

“Tukijiridhisha juu ya hayo mambo ndipo tutatoa hizo jezi kwa mawakala watakaoziuza kwa wateja wote, hata wale watakaokuwa wanauza rejareja watazingatia masharti hayo maana tukimkamata mtu anauza jezi feki basi huyo sheria itachukuwa mkondo wake.”

KUBANA MPAKANI

Meneja huyo wa GSM, aliongeza katika kudhibiti uuzwaji wa jezi feki wataandika barua mipaka yote ya nchi jiarani pamoja na kwenye mamlaka husika.

“Tutaziandikia barua mamlaka husika kama TRA, Bandari, Viwanja vya Ndege na mipaka mingine ya nchi zikiwemo mamlaka nyingine zinazojihusisha na biashara kuwa sisi ndio watu pekee tunaohusika na biashara ya jezi za Yanga.

“Ili ikitokea mtu ameingiza mzigo achukuliwe hatua, naamini tutafanikiwa kudhibiti hilo na watu watafuata sheria za biashara,” alisema meneja huyo.