Bigirimana aomba kuvunja mkataba

Muktasari:

Staa wa Stand United, Blaise Bigirimana raia wa Burundi  amesema si kweli juu madai yote yanayosemwa juu yake, na yamekua hivyo kwasababu anafatilia madai yake kwa uongozi kwa muda mrefu bila mafanikio.

BAADA ya kuona ataozea benchi kutokana na madai ya utovu wa nidhamu, mchezaji wa Stand United, Blaise Bigirimana raia wa Burundi amesema uongozi wa timu hiyo umekuwa ukimfanyia vituko vingi kwa madai ya utovu wa nidhamu.
Bigirimana alisema sio kweli madai yote yanayosemwa juu yake, na yamekua hivyo kwasababu amekuwa akifuatilia madai yake kwa uongozi kwa muda mrefu bila mafanikio na kupigwa chenga kila mara, hivyo wanatafuta njia ili aonekane hana nidhamu.
"Ndugu yangu hapa shida ni kubwa sana, nimedai madai yangu kwenye timu lakini mwisho wa siku wakaniambia tunakusimamisha miezi sita wakieleza kuwa nagoma kucheza wakati sio kweli,"
"Ninachotafatu kwa sasa ni kupata mtu atakayenisaidia kuandika barua vizuri ili niiwasilishe TFF kwa sababu nimegundua wanataka kuniacha baada ya dirisha la usajili kufungwa ili wanikomoe, hivyo bora nivunje mkataba nao kabisa," alisema Bigirimana.
Hata hivyo aliongeza anashaanga kutopewa barua hadi leo ya kusimamishwa kwani hata kwenye mazoezi anakwenda na kuna muda anaombwa kucheza lakini mchezaji huyo amegoma mpaka alipwe fedha zake zote.
"Nilisajiliwa kwa dau la Sh 5milioni pamoja na mshahara wa Sh 600,000 lakini hadi sasa wamenilipa Sh 2,500,000 pekee na sijapokea mshahara wa miezi nane, ninajua hawawezi kunilipa ndio maana naomba kuvunja nao mkataba,"
Alisisitiza anaiomba TFF imsaidie kwa sababu hajui lolote linalotakiwa kufanyika kutokana na ugeni wake na hajui wapi kwa kukimbilia zaidi ya TFF kama wazazi wa wachezaji wote.
Alisisitiza kuwa hata juzi Jumatano kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting walipolala kwa kufungwa mabao 2-1 aliamua mwenyewe kucheza na sio shinikizo la uongozi wa timu hiyo na sasa amebakiza vitu vichache kufikia kuvunja mkataba wake uliobaki miezi sita.
Meneja wa timu hiyo, Fredy Masai alipoulizwa juu ya hayo madai alisema wameyamaliza na hata adhabu ya kusimamishwa mchezaji huyo imekwisha ndio maana juzi alicheza.
Mchezaji mwingine, Sixtus Sabilo naye ameondoka kambini kwa madai ana matatizo ya kifamilia. "Ni kweli nimeondoka kambini, lakini nimetoa taarifa, hivyo ruhusa yangu haikutaka mtu kukubali au kukataa ila kwa sasa nipo nyumbani na nitarejea baada ya mapumziko mafupi," alisema Sabilo.
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zinaeleza Sabilo ni miongoni mwa wachezaji ambao anadai hivyo ameshindwa kuvumilia.