Big & Rick Ross hawa jamaa ni Simba hadi basi

UKISOMA kwa haraka haraka majina yao ya Big na Rick Ross, mawazo yanaweza kukupeleka Marekani nyumbani kwa wanamuziki maarufu duniani, Notorius BIG (marehemu) na Rick Ross.

Lakini hawa si marapa, wa Marekani. Hawa ni mashabiki maarufu wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam na majina yao halisi Habib Othman ‘Big’ na Daud Hussein ‘Rick Ross’.

Kwa wapenzi wa soka kupitia luninga na wanaojitokeza viwanjani katika mechi za Simba, bila ya shaka si wageni wa sura za wawili hawa wenye miili jumba.

Aina yao ya ushangiliaji na hasa staili yao ya uvaaji kofia ile ya kipekee ndefu yenye rangi za jezi ya Simba, nyekundu na nyeupe daima vimekuwa vikivutia macho ya mashabiki wengine na kamera za wapigapicha mbalimbali wakiwamo wa televisheni ya Azam inayorusha moja kwa moja mechi za Ligi Kuu Bara.

Kati ya matukio ya karibuni zaidi yanayokumbukwa kuhusu Big na Rick Ross, ni lile la wawili hao pamoja na mashabiki wenzao wa Msimbazi kushambuliwa na mashabiki wanaosemekana kuwa wa Yanga wakati wa mechi ya Wanajangwani dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Mwanaspoti ilifanya mazungumzo na wawili hao kwa nyakati tofauti na walikuwa na mengi ya kueleza kuhusu urafiki wao, maisha yao ya kawaida, familia na mapenzi kwa klabu ya Simba na tukio la kuchezea vitasa Morogoro na kukiri ‘Wananchi pale Jamhuri waliwapiga kama wezi, licha ya kubisha (kupambana)’.

Kwanza Mwanaspoti lilimtembelea Big katika shughuli zake za kutafuta riziki zilizopo Tandika-Mwisho na kufunguka aliyopitia kwa kupenda kwake soka na baadaye kuzungumza na Rick Rose na kila mmoja kuanika mambo yake ikiwamo gharama wanazozitumia na jinsi familia zao zinavyowachukulia.

Mbali na hayo, lakini walifichua namna wasivyoweza kusahau tukio la mjini Morogoro baada ya Wananchi, yaani mashabiki wanaodaiwa kuwa ni wa Yanga kuwapiga kama wezi, ilihali walikuwa kwenye burudani ya soka na kwa maisha yao ya kishabiki wamekuwa wakitaniana na wenzao kiroho safi...Ebu endelea nao!

MSIKIE BIG

Big ambaye ni baba mzazi wa watoto wawili Kaylar na Ashiraf, kati ya mambo ambayo anasema hawatakuwa tayari kufanya ni kulipiza kisasi dhidi ya mashabiki wanaodaiwa wa Yanga waliowapiga na kuwafanyia vurugu katika viwanja mbalimbali.

“Nafahamu tulivyo mashabiki wa Simba, hatutakuwa tayari kulipiza kisasi kwa mikasa ambayo tunapitia dhidi ya mashabiki wa Yanga na tunawakaribisha katika mechi zetu ili wapate burudani ya soka la kuvutia wenye kuondoka na pointi tatu,” anasema.

“Kwa ambavyo naiona timu yetu ilivyo msimu huu na tunavyoendelea kujipanga katika pambano la Novemba 7, baada ya kuahirishwa Oktoba 18, wasipoangalia tunaweza kuwafunga mabao mengi zaidi ya yale kwenye mechi iliyopita,” anasema Big.

SHANGWE MSIMBAZI

Big anasema alianza kuishangilia Simba tangu kinda, akiwa kijijini kwao Kibiti alipokuwa Shule ya Msingi tena wakati huo mechi zilikuwa hazionyeshwi kupitia luninga.

Anasema enzi hizo mechi hazikuwa zikionyeshwa, hivyo alikuwa anatumia ujanja wa kwenda na redio shule kwa kificho ili muda wa mechi utakapofika aweze kuweka sehemu ambayo mchezo unatangazwa.

“Nilikuwa naumia tangu nikiwa mdogo tena kabla ya kuanza shule nikiona Simba imefungwa hali hiyo nilijikuta nakwenda nayo mpaka katika elimu yangu ya msingi na maisha kwa ujumla mpaka sasa.”

“Mpaka nakuja hapa mjini kutoka nyumbani Kibiti nilikuwa sikubali kuona Simba wanacheza hapa Dar es Salaam halafu nashindwa kwenda uwanjani na kuna siku nilikuwa natoroka mpaka kazini mpaka mabosi zangu wanakasirika.

“Siku nyingine hata kama nilikuwa na pesa imebaki hiyo hiyo nilikuwa nalipa kiingilio ili nikaione timu yangu na baada ya mechi kuisha nilikuwa natembea kwa miguu kurudi nyumbani Mbagala,” anasema Big.

WAKE ZAO SASA

“Huwa napata wakati mgumu kwenda mkoani kuishangilia Simba ikicheza maana na mke wangu hataki kusikia wala kuona namuacha pamoja na watoto halafu mimi sipo,” anasema Big.

“Muda mwingine huwa natumia uamuzi kama baba wa familia kwenda katika mechi za mikoani bila kumuomba kibali mke wangu kwani amekuwa hapendi na huchukia mara zote ikiwa hivyo,” anasema.

“Kuna wakati huwa namuaga ananipa ruhusa ya kwenda, ila kwa shingo upande na huwa hakuna jinsi kwa kuwa Simba ni kitu kimoja cha mbele kabisa kati ambavyo navipenda. Mke wangu akikasirika mimi kuifuata Simba mkoani watoto zangu wawili akiwamo Kaylah (4), ambaye ndio wa kwanza huwa ananipa nguvu na kunibariki kama ambavyo huwa anakubali kuondoka sebuleni au ninapobadili chaneli ya luninga ili kuangalia mechi ya Simba.”

Kwa upande wa Rick Ross anasema mkewe ni shabiki wa Yanga tena yule wa kupindukia kwa maana hupenda kwenda uwanjani kushuhudia timu hiyo ikiwa inacheza, ila watoto wake wote watano ni mashabiki wa Simba.

Rick Ross anasema ikitokea siku Yanga inacheza mahala popote pale na anatamani kwenda huwa anamwambia na kumpatia mpaka nauli kwenda kushuhudia timu yake ambayo anaipenda.

“Kama ikitokea Simba na Yanga zinacheza kila mmoja anaondoka hapa nyumbani Chalinze akiwa na gari ambalo lina mashabiki wa upande wake na ikitokea kuna moja imefungwa na tukikutana hapa nyumbani hakuna kutaniana wala kuzungumzia suala lolote la mpira,” anasema.

“Habari zote za soka tunaziacha huko uwanjani na kila mmoja anatimiza majukumu yake kama baba na mama ili kuhakikisha majukumu na mambo ya kifamilia yanakwenda kama vile tunavyokubaliana.”

ILE KOFIA NDEFU

Rick Ross anasema ile kofia yake maarufu yenye rangi nyekundu na nyeupe ni ubunifu wake mwenyewe alioufanya kwa nia ya kutaka kujitofautisha na mashabiki wengine.

“Kila nikienda uwanjani nilikuwa naona mashabiki wanajichora rangi za timu zao, wengine wanatia matambara waonekane wana matumbo makubwa na kadhalika. Nikapata wazo la kutengeneza kofia ya kipekee initofautishe. Nikampelekea fundi wazo na maelekezo akanishonea vile,” anasema Rick Ross.

“Mke wangu ndio amekuwa akinifulia ile kofia yangu ambayo naivaa katika mechi zote ambazo nakuwa uwanjani na ni yeye ambaye huniwekea nguo za kuvaa safarini ninapojiandaa kuondoka kuifuata Simba. Haimsumbui licha ya kuwa yeye ni Yanga,” anasema Rick Ross.

GHARAMA ZA KUSAFIRI

Big anasema kati ya mambo yanayomsukuma kufanya kazi kwa nguvu ni gharama anazotumia kuifuata Simba inapocheza nje ya Dar es Salaam.

Anasema hana vipato vikubwa ila ambacho huwa anafanya katika biashara zake na shughuli zake nyingine kufanya kwa nguvu zaidi ili kupata pesa ya kutosha.

“Baada ya kufosi katika shughuli zangu napata pesa ya kuacha nyumbani kujikimu na ile ambayo nitaitumia katika safari zangu za mkoani na hii huwa haina kiasi maalumu kwani safari ni tofauti,” anasema Big, huku Rick Ross akisema kwa upande wake;

“Gharama inakuwa tofauti kwa kila mechi kwani inaweza kutokea Simba ikawa inacheza Dar es Salaam jioni muda ambao mechi ikimalizika naweza kupata usafiri kwa urahisi na nikarudi zangu nyumbani Chalinze siku hiyo hiyo. Wakati mwingine unalazimika kulala hotelini” anasema.

KIPIGO CHA MORO

Big anasema waliamua kwenda Moro kuangalia mechi ya Yanga na Mtibwa, kwa vile ilikuwa ni siku ya mapumziko, lakini wakashangaa mashabiki kuwatuhumu visivyo kuwa walienda kuwafanyia imani mbaya na kuanza kuwashambulia.

“Kiukweli Wananchi (mashabiki wa Yanga) walitupiga kama wezi. Kuna baadhi ya wenzetu waliumia na walikwenda hospitali kwa matibabu zaidi na jambo jema askari polisi wametuambia hatua kali zitachukuliwa dhidi ya waliofanya tukio hilo,” anasema Big.