Bifu za uwanjani za mastaa waliotamba Ligi Kuu England hizi hapa

Muktasari:

Hawa hapa mastaa waliokuwa na bifu kali ndani ya uwanja na kila walipokutana ilikuwa shughuli pevu.

LONDON, ENGLAND . MECHI za derby kwenye soka zina mvuto mkubwa kuzitazama. Zimekuwa na upinzani mkali na kila timu inajaribu kupambana isipoteze mchezo.

Ni kitu cha wazi kuona upinzani mkali Manchester United inapocheza na Manchester City, Liverpool na Everton, Arsenal na Tottenham Hotspur, Liverpool na Man United au Sunderland na Newcastle United. Inakuwa vuta nikuvute.

Lakini, kuna upinzani mwingine kwenye soka unaowahusisha mchezaji mmoja mmoja. Kwenye Ligi Kuu England kuna mastaa hao walikuwa na bifu na kila walipokutana ndani ya uwanja ilikuwa balaa kubwa.

Hawa hapa mastaa waliokuwa na bifu kali ndani ya uwanja na kila walipokutana ilikuwa shughuli pevu.

Jamie Carragher & Gary Neville

Utashangaa kwa sasa kuona wawili hao wakiwa marafiki na kufanya kazi ya uchambuzi wa soka kwenye televisheni. Lakini, walipokuwa wakicheza, wawili hao walikuwa maadui wakubwa na wenye bifu kali. Shida ni wachezaji hao kila mmoja alikuwa akiipenda sana timu yake anayochezea na Neville alikuwa Manchester United na Carragher ni Liverpool na kama inavyofahamika upinzani wa timu hizo mbili zinapokutana. Jambo hilo lilifanya Neville na Carragher kuwa kwenye bifu kali.

Fernando Torres & Nemanja Vidic

Nemanja Vidic alikuwa mmoja wa mabeki bora kabisa waliowahi kutokea kwenye Ligi Kuu England. Lakini, ubora wake wote alikuwa akipata shida sana alipokutana na straika Fernando Torres. Kipindi ambacho Torres alikuwa Liverpool, alimsababishia Vidic kutolewa nje mara mbili kwa kadi nyekundu, ilikuwa 2008. Wawili hao walikuwa kwenye bifu kubwa na iliendelea kuwa hivyo hata Torres alipohamia kwenye kikosi cha Chelsea na ilikuwa balaa uwanjani Stamford Bridge 2014.

Alan Shearer & Roy Keane

Mastaa hawa wawili walikuwa ngumi mkononi. Kila walipokutana basi ilikuwa balaa kubwa ndani ya uwanja. Mambo yalianzia mwaka 2001, wakati Keane alipomkosa kwa konde kali straika Shearer. Baada ya hapo, yaliibuka majibizano makubwa kwenye korida za kuingilia vyumbani. Shearer alikwenda kulipa kisasi ndani ya uwanja kwa kupiga kiwiko katika mechi iliyopigwa uwanjani Old Trafford. Wawili hao walikuwa kawatazamani usoni hadi walipostaafu soka.

Ian Wright & Peter Schmeichel

Ilianza kwa madai kwamba Wright amefanyiwa vitendo vya kibaguzi na kipa Schmeichel. Jambo hilo likazua chuki na bifu kubwa baina ya wachezaji hao na kila walipokutana kwenye mechi basi ilikuwa vita kubwa. Schmeichel alisafishwa hakutenda kitendo chochote cha kibaguzi, lakini hilo halikumaliza bifu la wawili hao wakati Arsenal ilipomenyana na Man United. Kuna mechi moja iliyofanyika Highbury, Wright alimchezea rafu mbaya Schmeichel kwa kumrukia miguu miwili. Kwa sasa wapo vizuri.

John Terry & Wayne Bridge

Bifu nyingine za wachezaji zimekuwa zikizaliwa ndani ya uwanja tu, lakini hii ya John Terry na Wayne Bridge imetokea nje ya uwanja. Kabla ya hapo, wawili hao walikuwa marafiki wakubwa, lakini mambo yaliharibika baada ya Terry kuwa na uhusiano wa kimapenzi na aliyekuwa mchumba wa Bridge, mrembo Vanessa Perroncel. Jambo hilo lilianzisha bifu kubwa baina ya wachezaji hao wawili ambao wote walikuwa wakiichezea timu ya taifa ya England. Terry alivuliwa unahodha wa England kisa bifu hilo.

Roy Keane & Patrick Vieira

Hili bifu lilikuwa utamu wenyewe wa mechi za Manchester United na Arsenal. Kila mechi hizo mbili zilipofanyika, basi walichokuwa wakikifikiria watu ni shughuli itakayoonyeshwa na manahodha wawili, Roy Keane na Patrick Vieira. Ilikuwa ubabe. Keane akimchezea rafu mchezaji yeyote ya Arsenal, Vieira alikuwa akilipa kwa mchezaji wa Man United. Kukunjana jezi ndani ya uwanja kilikuwa kitu cha kawaida kwa wachezaji hao kwenye mechi zao.

Diego Costa & Yeyote

Kuna kundi kubwa la wachezaji waliowahi kulumbana na straika Diego Costa. Ni wachezaji kibao wamelumbana na straika huyo, lakini bifu lake dhidi y beki wa zamani wa Liverpool, Martin Skrtel lilikuwa balaa zaidi. Wawili hao walipokutana, ilikuwa balaa. Ilikuwa vuta nikuvute, viwiko, kuvutana kukanyagana na vurugu za kila aina.

Mashabiki walivutiwa na bifu lao kwa sababu liliwakutanisha mastaa wawili waliokuwa wakorofi na uhuni mwingi.