Bibi Cheka aibuka, adai kudhulumiwa TMK Wanaume

Monday September 3 2018

 

By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Msanii wa Bongo fleva, Cheka Hija 'Bibi Cheka', amedai kutekelezwa na uongozi wa Wanaume TMK kwa kushindwa kutekeleza mkataba waliokubaliana wa kumjengea nyumba ya kisasa.

Akizungumza na MCL Digital, nyumbani kwake Bunju, Bicheka aliyepata umaarufu kutokana na kuwa msanii mwenye umri mkubwa katika muziki huo wa kizazi kipya, amesema wakati alipokuwa akisimamiwa na kundi hilo mojawapo ya makubaliano chini ya  uongozi wa Said Fella 'Mkubwa Fella' ilikuwa kumjengea nyumba ya kisasa.

Badala yake walivyoachana naye tangu miaka minne iliyopita, uongozi huo walichokifanya ni kumpatia matofali 400 na mifuko ya cement 50 na kulipa hela ya fundi Sh150,000 ambayo ilimwezesha kujenga nyumba ya vyumba vitatu iliyofika usawa wa linta.

"Kwa kuwa nilikuwa naishi bado kwenye nyumba ya udongo na familia yangu ya watoto wawili na wajukuu zangu, ilinibidi niuze kipande cha ardhi hapa kwangu ili kuweza kumalizia nyumba hiyo ambayo ndiyo naiishi sasa," amesema msanii huyo aliyewahi kutesa na kibao cha 'Ni wewe' akimshirikisha Mh. Temba.

Aliongeza kuwa katika mwendelezo wa kundi hilo kutomjali, hata alipougua na kushindwa kuendelea na kazi za muziki kwa muda, haukumjali hata kwenda kumuona na mpaka leo hana mawasiliano nao.

Akizungumzia hilo, Mkubwa Fella amesema hakuwa na mkataba wowote na bibi hiyo wakati akiwa anafanya kazi katika kundi hilo la TMK, zaidi alimsaidia baada ya kumuomba ili aweze kujikimu kimaisha.

"Bicheka sijawahi kumsainisha kokote kama msanii wangu, nilichokifanya ni kumpa msaada baada ya kuja kwangu ili na yeye aweze kuendesha maisha yake kutokana na kuja kwangu akilia ana shida.

"Pamoja na usamaria wangu huo nilijikuta nikibeba lawama kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini kwamba ninavyomvalisha bibi huyo suruali, fulana na kofia namdhalilisha bila kujua ni yeye mwenyewe alikuwa anapenda kuvaa vile, ila yote nilikaza roho kwa kuwa nilikuwa nazijua shida alizo nazo," amesema Fella.

Hata hivyo Fella amesema kwa bahati mbaya wakati akiwa anamfanyia hisani hiyo, kuna watu walimdanganya bibi huyo kwamba watamsimamia katika muziki wake na hapo ndipo ikawa chanzo cha yeye kuondoka katika usimamizi wake jina lake kupotea.

Hata hivyo amekiri wao kama TMK waliamua kumpa msaada huo wa matofali na cement ili kujenga kibanda cha kujisitiri na wala haikuwa ni mkataba kwamba lazima wamjengee kama alivyodai bibi huyo.

Kuhusu kutokwenda kumjulia hali alipokuwa mgonjwa, Mkubwa Fella amesema imetokana na kubanwa na majukumu mengi ya kazi za kimuziki na kuwatumikia wapiga kura wake wa Kata ya Kilungule.

Advertisement