Biashara waivimbia Simba Dar

Wednesday September 16 2020

By OLIVER ALBERT

KOCHA wa Biashara united, Francis Baraza amesema wataikabili Simba kwa kuwapa heshima yao kama timu nzuri, mabingwa watetezi lakini hawawaogopi hata kidogo.

Biashara United itatua Dar es Salaam kesho Alhamisi tayari kuikabili Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa.

Baraza ambaye ameiongoza timu yake kushinda mechi zote mbili za Ligi Kuu Bara msimu huu alisema anajua ubora na udhaifu wa Simba hivyo anayafanyia kazi mambo hayo ili kuhakikisha anaondoka na pointi tatu ugenini.

Timu hiyo ilianza Ligi kwa kuichapa Gwambina bao 1-0 kisha ikapata ushindi kama huo kwa kuifunga Mwadui Jumapili iliyopita.

“Nimengalia mechi zao zote mbili za Simba licha ya kwamba wameanza kwa kusuasua kwa kushinda mechi moja na sare moja lakini hilo halitufanyi tuzembee kwani Simba ni Simba huwezi jua watakuja vipi kutukabili.

“Tunakutana na timu kubwa yenye historia ya nchi hii hivyo lazima tuwape heshima yao na tutawakabili kwa uangalifu lakini pia wajue hatuwaogopi,”alisema Baraza raia wa Kenya.

Advertisement

“Simba wako vizuri zaidi hasa kwenye kiungo lakini pia ni timu inayoshambulia kwa pamoja na kulinda pamoja hivyo kupambana na timu kama hiyo lazima ujipange sana hivyo lazima nifanye kitu katika timu yangu kuhakikisha tunawadhibiti kwani tunataka tuendeleze moto wetu wa kuvuna pointi kila mchezo.

“Licha ya kwamba muda utakuwa mchache kutokana na umbali wa mahali tunapotoka lakini tunaamini siku hizo mbili tutafanya mazoezi vizuri yatakayotuweka tayari kwa ajili ya mchezo huo,”alisema Baraza.

Advertisement