Biashara United kuhitimisha na Tusker

Monday August 12 2019

 

By OLIVER ALBERT

BIASHARA United leo Jumatatu saa 10:00 jioni itaumana na Tusker ya Kenya katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika Uwanja wa Karume  wilayani Musoma mkoa wa Mara.
Timu hiyo nayoshiriki Ligi Kuu Bara itacheza mchezo huo ukiwa ni maaalum kwa ajili ya kukamilisha kilele cha siku ya Biashara United ambayo pia itatumika kuzindua jezi na kutambulisha wachezaji wapya wa kikosi hicho.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Seleman Mataso amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu yao na kushuhudia kikosi kipya cha maangamizi kitakachouwakilisha mkoa huo kwenye ligi msimu mpya utakaoanza Agosti 23 mwaka huu.
"Nawaomba mashabiki wetu kutoka mkoa wa Mara na hata mikoa ya jirani kufika kwa wingi ili kuja kuishuhudia timu yao na  pia kuona usajili wa wachezaji wapya"amesema Mataso.
Kiingilio katika mchezo huo kitakuwa Sh 10,000 kwa VIP na 5000 kwa mzunguko wakati watoto ni sh 2000.
Biashara United  msimu ujao utakuwa ni msimu wake wa pili kwenye Ligi Kuu Bara tangu ilipopanda daraja mwaka 2017 na iliponea chupuchupu kushuka daraja msimu uliopita baada ya kufanya vibaya katika michezo yake mingi.
Timu hiyo inanolewa na beki wa zamani wa Simba na timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Amri Said'Jap Stam'.

Advertisement