Biashara United, Mbao FC kukiwasha Nanenane

Tuesday August 7 2018

 

By Masoud Masasi

Mwanza. Biashara United iliyopanda Ligi Kuu Bara msimu huu itacheza mechi yake ya kirafiki dhidi ya  Mbao FC kesho katika kujiandaa na msimu mpya.
Mtanange huo unatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Musondore Mugango wilayani Musoma mkoani humo ukiwa ni maalumu kwa timu hizo kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu.
Kocha Mkuu wa Biashara United, Hitimana Thierry alisema mechi hiyo itampa nafasi kubwa kuwapima wachezaji wake kiubora kabla ya Ligi Kuu kuanza.
Alisema kuwa wameamua kucheza na timu hiyo ili kupata ushindani kutokana na Mbao imekuwa na rekodi nzuri ya ushindani tangu ilipopanda Ligi Kuu.
“Ni mchezo muhimu kwangu kutambua uwezo wa vijana wangu, Mbao tunaiheshimu, hivyo nitautumia mpambano huo kuwasoma vijana wangu kinidhamu na kiufundi,” alisema Thierry.
Kocha wa Mbao, Amri Said ‘Stam’ alisema  katika mechi mbili walizocheza na kushinda, lakini mechi hiyo anaipa umuhimu katika kuona uwezo wa wachezaji wake.
 “Tumecheza mechi mbili na timu ndogo na tumeshinda zote, lakini lengo langu ni kusuka timu yenye ushindani, ambayo muda wote itanipa matokeo mazuri, mchezo wa kesho nitawaona vijana uwezo wao,”alisema Kocha huyo.

Advertisement