Biashara, Alliance FC ni vita Kanda ya Ziwa

Muktasari:

Hata hivyo Biashara United wanawakaribisha wapinzani hao wakijivunia rekodi nzuri ya kutopoteza mechi yoyote nyumbani tangu wamwajiri Mkenya, Francis Baraza ambaye ameongoza mechi sita ikiwamo moja ya FA.

HUKO Musoma lazima kieleweke kutokana na makocha wa timu za Biashara United na Alliance FC kusisitiza kuwa wanahitaji pointi tatu katika mchezo wa Ligi Kuu utakaopigwa leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma.
Timu hizo zinakutana, huku kila upande ukikumbuka ushindi kwenye mechi iliyopita, ikiwa Alliance alishinda ugenini dhidi ya Kagera Sugar mabao 2-1 na Biashara wakitakata kwa Mbao bao 1-0.
Hadi sasa Biashara United wako nafasi ya 10 kwa pointi 28 na wapinzani wao wakiwa na alama 25 nafasi ya 13 baada ya kucheza mechi 21 kila timu.
Hata hivyo Biashara United wanawakaribisha wapinzani hao wakijivunia rekodi nzuri ya kutopoteza mechi yoyote nyumbani tangu wamwajiri Mkenya, Francis Baraza ambaye ameongoza mechi sita ikiwamo moja ya FA.
Kocha Mkuu wa Alliance FC, Fredy Felix ‘Minziro’ alisema wanawaheshimu wapinzani, lakini hawawaogopi na wanaenda kupambana kusaka pointi tatu ili kujiweka pazuri kwenye msimamo.
“Tumetoka ugenini mjini Bukoba licha ya uchovu lakini tulishinda, kwahiyo hatuwezi kuwaogopa wapinzani isipokuwa nidhamu ya mpira na kupambana itatupa mafanikio” alisema Minziro.
Kwa upande wa Baraza alisema kikosi kipo fiti na wanachohitaji ni kuendeleza rekodi yao nyumbani, huku akifafanua kuwa hadi sasa ni mchezaji mmoja tu, Kelvin Friday ambaye hajakaa sawa.
“Mchezo utakuwa mgumu lakini nashukuru vijana wanapambana na wanasikiliza nini nahitaji, Friday ndiye bado hajapona majeraha lakini wengine wako fiti na tunatarajia pointi tatu” alisema Baraza.