Benki yatoa ushahidi kesi ya Aveva

Muktasari:

  • Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 10 na kuutaka upande wa mashtaka kuleta mashahidi ili imalizike kwa wakati.


MENEJA wa Benki ya Barclays Tawi la Mikocheni, Prisca Daudi, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa aliyekuwa Rais wa Simba, Evans Aveva ni mteja wa benki hiyo.

Prisca alidai hayo jana Jumatatu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati akitoa ushahidi.

Akiongozwa na Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Leonard Swai, Prisca alidai Aveva ni mteja wake ambapo alifungua akaunti katika Tawi la Mikocheni.

Alidai katika taratibu za kufungua akaunti mteja anatakiwa kupeleka picha yake ili kujua kama yeye ndiye mhusika, kitambulisho pamoja na barua kutoka serikali ya mtaa au kwa mwajiri wake.

Shahidi huyo aliendelea kudai Novemba 20, 2014, Aveva alifungua akaunti iliyokuwa na nyaraka kutoka klabu ya Simba ikionyesha kipato chake kwa mwezi ni Sh 8.8 milioni. Prisca alidai Machi 16, 2016 ziliingia pesa kwenye akaunti ya mteja wake ambaye ni Aveva kiasi cha Dola 300,000 kutoka Benki ya CRDB.

Alidai fedha zinapozidi kiasi kwenye akaunti ni lazima kukaa na kujiridhisha pesa hizo ni za nini. Prisca, ambaye ni shahidi wa tatu, alidai fedha hizo zilionyesha ni malipo ya mkopo kutoka Benki ya CRDB kwenda akaunti ya Aveva. Alidai Aprili 4, 2016 kiasi cha Dola 620,000 zilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya Aveva na kulipwa kwenye Kampuni ya China kwaajili ya kulipia nyasi.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 10 na kuutaka upande wa mashtaka kuleta mashahidi ili imalizike kwa wakati.

Mbali na Aveva vigogo wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Makamu wa wake, Geofrey Nyange maarufu (Kaburu) na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe.