Bendera ameondoka na rekodi yake Taifa Stars Lagos 1980

Muktasari:

>> Taifa Stars wakati huo ikiwa chini ya Kocha, Slowmir Work kutoka Poland, akisaidiwa na Joel Bendera na Ray Gama, ilikata tiketi ya kushiriki Fainali hizo za Afrika

UKIZUNGUMZIA Fainali za Afrika mwaka 1980 zilizofanyika Lagos, Nigeria, ambazo Tanzania ilishiriki kwa mara ya kwanza na mwisho, huwezi kuacha kumtaja Joel Nkaya Bendera.

2017 ni miaka 37 tangu timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kucheza fainali hizo za Afrika rekodi ambayo haijavunjwa na kocha yeyote aliyeiongoza timu hiyo. Kwa mara ya kwanza na mwisho, Tanzania iliingia fainali hizo za Afrika 1980 na kwa mara ya kwanza ilicheza michuano ya Afrika kwa wachezaji wa ndani, Chan, fainali zilizofanyika kwa mara ya kwanza Ivory Coast 2009.

Katika michuano hiyo ya 1980, wenyeji walitwaa ubingwa na wakati huo michuano ilikuwa ikiwakilishwa na timu 12. Kwa sasa fainali za Afrika zinashirikisha mataifa 24 baada ya Rais wa sasa Ahmad Ahmad kubadilisha utaratibu.

*SAFARI YA STARS LAGOS 1980

Taifa Stars wakati huo ikiwa chini ya Kocha, Slowmir Work kutoka Poland, akisaidiwa na Joel Bendera na Ray Gama, ilikata tiketi ya kushiriki Fainali hizo za Afrika ambazo sasa kila mmoja ana kiu ya kuona Tanzania kwenye luninga ikicheza fainali hizo kwa mara nyingine.

Itakumbukwa Agosti 26,1979 wakati Taifa Stars ilipokuwa ikirudiana na Zambia enzi hizo ikiitwa ‘KK Eleven’ katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu Fainali za Afrika za mwaka 1980 zilizofanyika Lagos, Nigeria.

Katika pambano hilo lililochezwa mjini Ndola, nje kidogo ya jiji la Lusaka, Taifa Stars ilikuwa ikihitaji sare ya aina yoyote ili ifuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza tangu ilipoanza kushiriki mwaka 1968.

Timu hizo zilikuwa zinarudiana baada ya wiki mbili za mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Taifa Stars kuilaza Zambia bao 1-0 lililofungwa na kiungo, Mohammed Rishard Adolph.

Katika mchezo huo wa marudiano, ‘Kenneth Kaunda Eleven’ walipata bao la mapema katika mchezo huo ambalo lilidumu hadi dakika ya 85.

Dakika tano za mwisho, mshambuliaji wa Pan African wakati huo, Peter Tino alibadili sura ya mchezo kwa kusawazisha bao na kunyamazisha umati wa mashabiki waliofurika kwenye Uwanja wa Ndola.

Katika mchezo huo, ilipigwa kona kuelekezwa lango la Stars, lakini kipa wake, Juma Pondamali ‘Mensar’ akaupangua kwa ngumi, ukamkuta kiungo Leodegar Tenga ambaye naye alitoa pasi ndefu kwa Hussein Ngulungu ambaye naye alimgongea pasi ndefu Tino aliyeukwamisha kimiani.

Tino aliwatoka mabeki hao na alipofika nje kidogo ya eneo la hatari la Zambia, alitandika kombora la mguu wa kulia, lililompita kipa wa Zambia aliyekuwa kikwazo, John Shileshi.

Katika mchezo ule Tanzania iliwakilishwa na Juma Pondamali aliyekuwa langoni, Leopard Tasso, Mohammed Kajole/ Ahmed Amasha, Salim Amir, Jella Mtagwa, Leodegar Tenga, Hussein Ngulungu, Omari Hussein, Peter Tino, Mohamed Salim na Thuweni Ally.

*FAINALI ZA LAGOS SASA

Katika fainali hizo, Taifa Stars ilichapwa mabao 3-1 na wenyeji Nigeria katika mechi ya ufunguzi, ikatoka sare ya mabao 2-2 na Ivory Coast kabla ya kuchapwa mabao 2-1 na Misri na kutolewa hatua ya makundi.

Kwa sasa, imepangwa Kundi L pamoja na Uganda, Cape Verde na Lesotho kuwnaia kucheza Fainali za Afcon 2019 za Cameroon.

KWAHERI JOEL BENDERA

Bendera alifariki jana dunia jana Alhamisi kwenye hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam.

Bendera alikumbwa na mauti hayo jioni ya jana ikiwa ni saa nne tu tangu apopokewa Muhimbili akitokea mjini Bagamoyo.

Akizungumza jana jioni, Msemaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, MNH, Aminiel Aligaesha alithibitisha kifo cha mwanamichezo huyo maarufu wa zamani aliyekuwa pia mwanasiasa.

“Ni kweli Joel Bendera amefariki. Aliletwa leo na gari la wagonjwa akitokea hospitali ya Bagamoyo saa 6.30 mchana na ilipofika saa 10.24 jioni alifariki.” Mwanaspoti lilipotaka kujua chanzo cha kifo chake alisema; “Hilo sasa ni suala la familia lakini kwa wakati huu itoshe kusema amefariki.”

Bendera ambaye ni mwanamichezo enzi za uhai wake alipata kushika nyadhifa za ubunge wa Korogwe Mjini, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo katika utawala uliopita wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Katika mabadiliko ya wakuu wa mikoa yaliyofanywa na Rais John Magufuli Oktoba 26, Bendera alikuwa miongoni mwa wakuu wa mikoa waliostaafu na nafasi yake ikichukuliwa na Alexander Mnyeti aliyepandishwa kutoka Mkuu wa Wilaya ya Arumeru.