Benchi la Yanga lamliza Mwinyi

Muktasari:

Mwinyi pamoja na kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza cha Mwinyi Zahera bado anaamini uwepo wa timu 20 unampa imani ya kupata nafasi ya kucheza na kwamba atarejea kwenye kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars'

BEKI wa Yanga, Haji Mwinyi amekiri kiwango cha beki mwenzake, Gadiel Michael kipo juu mno, ndio maana anapata nafasi ya kucheza, ila amempasha kocha wake Mwinyi Zahera siku akijiroga na kumpa nafasi ya kucheza hatafanya makosa kwani benchi limemchosha.

Mwinyi, kwa sasa hana nafasi katika kikosi cha Zahera na tangu Gadiel asajiliwe Yanga amegeuka kuwa mwiba kwake kwa kuingia kikosi cha kwanza huku yeye akipotezewa, jambo linalomuuma kwa vile soka ni ajira yake na angependa acheze mra kwa mara.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwinyi alisema bado ana uwezo wa kucheza kama ilivyokuwa zamani, ila tatizo ni jinsi ya kupata nafasi, ila alisema endapo atapata nafasi atafanya kweli na utakuwa mwanzo wa kurudisha jina lake ndani ya Yanga na Taifa Stars.

Beki huyo alisema changamoto hiyo ya kuwekwa benchi inampa wakati mgumu kwani anaamini ana uwezo wa kuisadia Yanga kwa sasa kufanya vizuri na kuongeza kukaa benchi kunamuongeza nguvu za kupambana zaidi.

“Sina bahati na Zahera najaribu kumshawishi na naendelea kufanya hivyo lengo langu ni moja tu kumfanya anipe nafasi ya kuonyesha uwezo wangu uko wapi pia itamsaidia kufahamu utofauti wangu na Gadiel,” alisema Mwinyi akiwa na tabasamu hafifu.