Beki wa Stars awapania Sudan

BEKI wa Taifa Stars, Idd Mobby amesema wapo tayari kulipambania taifa lao kuhakikisha wanaibuka na ushindi dhidi ya Sudan katika mechi ya kesho Jumapili ya kuwania kufuzu fainali za AFCON.
Amekiri mechi hiyo itakuwa ya ushindani wa hali ya juu, lakini anaamini wana nafasi kubwa ya kushinda nyumbani na kinachompa kujiamini ni maandalizi waliofanya chini ya makocha wao Etienne Ndayiragije akisaidiana na Juma Mgunda pamoja na Seleman Matola.
Amesema wana ujasiri na ari ya kuhakikisha wanatimiza malengo ya kujitengenezea ushindi nyumbani kabla ya mechi ya marudiano itakayochezwa Sudan.
"Haitakuwa mechi rahisi, tuna kila sababu ya kushinda kwa sababu sisi ndio wenyeji wa mchezo huu, pamoja na hilo hatujabweteka tumejiandaa vya kutosha"
"Mazoezi tuliofanya ni ya mbinu kutokana na kocha kuwatazama wapinzani wetu walivyo, naamini tutafikia malengo tunayoyahitaji"
"Mashabiki waje kwa wingi kutuunga mkono kwani tunategemea sapoti yao na hiyo ndio faida ya kucheza nyumbani, tupo tayari kuwapa raha"amesema.
Naye meneja wa timu hiyo, Nadir Haroub 'Cannavaro' amesema kwa namna ambavyo wachezaji wamejengwa kisaikolojia, mbinu walizopewa na kuwekwa kwenye mazingira mazuri anaona kwamba watafanya maajabu.
"Wachezaji watafanya kazi yao ya kulipambania taifa dhidi ya Sudan, pia mashabiki nao wawajibike kwa upande wao, wajitokeze kwa wingi kuhakikisha wanatoa sapoti yao ambayo ni muhimu sana"amesema.