Beki Simba ampa mchongo Yondani

WAKATI Juma Abdul akiziita mezani timu zenye nia ya kuhitaji huduma yake kisoka, Kelvin Yondani ameshauriwa kuangalia upepo mwingine nje ya nchi kama ana nia ya kuendelea kucheza soka.

Mabeki hao walishindwa kuafikiana na Yanga katika malipo ili kuongeza mikataba mipya wakati huu wa dirisha kubwa.

Akizungumza na gazeti hili jana, Abdul alisema yuko tayari kuichezea timu yoyote itakayomhitaji kama wataafikiana.

Alisema hadi sasa bado hajaamua muelekeo wake, lakini yuko tayari kujiunga na timu yoyote.

Ingawa hivi karibuni alihusishwa kutakiwa na na Azam na Namungo, Abdul alisema bado hajapata ofa hizo.

“Ikitokea zikanihitaji, sio hizo tu, timu yoyote ije tukae mezani niwape ofa yangu, tuelewane nianze kazi,” alisema.

Kwa upande wa Yondani, mwenye umri wa miaka 35, licha ya kukataa kuzungumzia hatma yake baada ya kushindwana na iliyokuwa klabu yake ya Yanga, beki wa zamani wa kimataifa wa Simba, Boniface Pawasa amemshauri mchezaji huyo kuangalia maisha mengine ya kisoka nje ya nchi japo kwa mwaka mmoja.

“Mpira wa Bongo una vikwazo vingi na ndicho kinatokea kwa Yondani na Abdul hivi sasa,” alisema Pawasa.

Alisema Yondani ni beki bora na amekuwa na msimu mzuri si Yanga tu hadi timu ya Taifa, kama ilivyo kwa Abdul ambaye amemtaja kuwa ni mpambanaji.

“Sijui nini kimewatokea Yanga, ila bado wana kiwango cha kucheza kwa miaka mitatu zaidi, wakiweza waende nchi kama Zambia au Rwanda angalau kwa mwaka mmoja kisha warudi, naamini ile heshima yao kisoka itarejea,” alisema.

Alisema mabeki hao hawapaswi kukata tamaa, kwani wachezaji wengi walikutana na vikwazo kama hivyo na baadhi kuacha soka mapema, ikiwamo yeye.

“Niliondoka nikaenda nje ya nchi, niliporudi nilipata nafasi ya kucheza nchini tena kwa kiwango kizuri tu sababu sikukubali kukatishwa tamaa,” alisema.