Beki Mwarabu azigonganisha KMC, Stand Utd

Wednesday July 11 2018

 

By Saddam Sadick

Usajili wa mchezaji Ally Ally “Mwarabu” aliyetua KMC umeishtua Klabu yake ya Stand United na kusema kuwa bado beki huyo ni mali yao kutokana na kuwa na mkataba nao wa miaka miwili na kwamba waliomsajili hawakufuata utaratibu.

Beki Ally aliyeitumikia Stand United msimu uliopita,tayari amemwaga wino kwa kandarasi ya mwaka mmoja kuichezea KMC katika msimu ujao wa Ligi Kuu.

Mwenyekiti wa Stand United, Elyson Maheja alisema kuwa wanachoamini beki huyo Mzanzibari ni mali yao na kama kuna klabu iliyomsajili bila utaratibu itakula kwao.

Alisema kuwa mchezaji huyo alisaini kandarasi ya miaka mitatu kuitumikia timu hiyo akitokea Gulioni FC ya Zanzibar, hivyo hadi sasa alikuwa na mkataba wa miaka miwili kuendelea na kikosi hicho.

“Sisi tunasikia hizo taarifa juu juu na hatujajua kama watakuja kuvunja mkataba au la,lakini niseme kwamba kama wamemchukua bila kufuata utaratibu itakula kwao kwa sababu kanuni ziko wazi,” alisema Maheja.

Kwa upande wake Afisa Habari wa KMC, Anwary Binda alianza kwa kuthibitisha kumsainisha chipukizi huyo kwa kandarasi ya mwaka mmoja na kwamba wao walijiridhisha kwa mchezaji huyo kuvunja mkataba na Klabu yake ya Stand United.

Alisema kuwa licha ya kumsainisha beki huyo alikiri kutokufanya mawasiliano na timu aliyotoka na kusema kuwa Klabu yao (KMC) itaendelea kufuatilia suala hilo na mambo yatakaa sawa.

“Ni kweli tumemsainisha mchezaji Ally, lakini hatujawasiliana na timu aliyotoka licha ya kujiridhisha kwake kuvunja mkataba, KMC italifuatilia suala hilo na mambo yatakuwa sawa”alisema Binda.

 

 

Advertisement