Beki 5 mpya Namungo anayemuwaza Kagere

Muktasari:

Hata hivyo, Toure hatapata fursa ya kumkabili Kagere hadi mwakani wakati timu hizo zitakapokutana kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu Bara msimu huu.

Baada ya kumaliza msimu uliopita akiwa mfungaji bora katika msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu ya Bara na kisha kuuanza msimu huu kwa moto uleule, si ajabu kwa kila mdau wa soka la Bongo kumuangalia kwa macho mawili-mawili straika wa Simba, Meddie Kagere ‘MK14’.

Na ndiyo maana huwezi kushangazwa na beki mpya wa Namungo ya Lindi, Toure Leopold, kumtaja straika huyo wa Rwanda katika malengo yake aliyojiwekea ya kuwapa wakati mgumu washambuliaji wote wa upinzani TPL.

Toure, beki wa kati anayetokea Ivory Coast, anasema amekuwa akisoma baadhi ya washambuliaji ili kujua namna gani ya kukabiliana nao watakapokutana msimu huu.

Muivory Coast huyo aliyewahi kutamba na Majees FC ya Oman, anasema amekuwa akijifua mara mbili kwa siku huku akijitengenezea utimamu wa mwili ili kukabiliana na washambuliaji hao ambao anadai namna yao ya uchezaji wamekuwa wakitumia nguvu nyingi.

“Nimemuona Kagere ni mchezaji mzuri mwenye uwezo wa kufunga kwenye mazingira yoyote kwa sababu ana nguvu, nimecheza dhidi ya washambuliaji wa aina yake katika nchini tofauti hivyo sina hofu ya kukutana naye.

“Nimecheza Oman, nikacheza DR Congo, Burkina Faso na Nigeria, kote huko nimepata uzoefu, kwa hiyo naamini naweza kukabiliana na mchezaji yeyote wa Ligi Kuu Tanzania,” anasema.

Hata hivyo, Toure hatapata fursa ya kumkabili Kagere hadi mwakani wakati timu hizo zitakapokutana kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu Bara msimu huu.

Beki huyo, anasema licha ya kuwa Namungo ni timu ngeni kwenye Ligi Kuu inaweza kufanya maajabu kutokana na aina ya wachezaji walionao, kwani asilimia kubwa wana vipaji vya hali ya juu.

Anasema kinachoweza kuwasumbua kwa kipindi kifupi ni kuwa na muunganiko kutokana na ugeni wa baadhi ya wachezaji, akiwamo yeye ambaye msimu huu atacheza kwa mara ya kwanza soka la Tanzania huku rafiki yake, Nouridine Abarola huu utakuwa msimu wake wa pili baada ya msimu uliopita kuichezea Biashara United ya Mara.

Namungo walianza na ushindi kwenye mechi yao ya kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya mahasimu wao wa kusini mwa Tanzania, Ndanda ya Mtwara kwa mabao 2-1.

Toure anasema, wakati Simba ina safu bora ya ushambuliaji, Yanga washambuliaji wao ni kawaida sana, pengine ni kutokana na ugeni wao kwenye klabu hiyo.

“Niliambiwa kuwa washambuliaji wa Yanga wengi ni wapya. Azam tulicheza nao mechi ya kirafiki, natambua ubora wao upo kwa wachezaji gani. Kinachoweza kuwa kipya kwangu ni kucheza dhidi ya timu za kawaida ambazo washambuliaji wake siwafahamu,” anasema Toure.

Nyota huyo anakuwa mchezaji mwingine kutoka Ivory kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, mwingine ni Pascal Wawa ambaye ni moja ya mabeki bora wa kigeni ambao wamecheza soka la Tanzania kwa mafanikio.

“Namjua Wawa na nimekuwa nikiongea naye, ni zaidi ya rafiki kwangu na kabla ya kujiunga na Namungo nilifanya naye mawasiliano akanikaribisha kwa moyo mmoja Tanzania,” anasema.

Toure alianzia maisha yake ya soka kwenye kituo cha Africa Sports d’Abidjan akiwa na Jean Michael Seri, Sylvain Gbohouo, Wilfried Kanon na Jonathan Zongo.

Wenzake hao kwa sasa ni wachezaji wenye majina makubwa, Seri ni mchezaji wa Fulham anayeichezea Galatasaray ya Uturuki kwa mkopo, Gbohouo ni kipa wa TP Mazembe, Kanon ambaye baadaye alijiunga na Empoli kwa sasa anaichezea ADO Den Haag ya Uholanzi, Jonathan Zongo anaichezea Army United ya Thailand.

Akizungumzia malengo yake, Toure anasema ni kuiletea heshima Namungo huku akionyesha uwezo wake ambao anaamini unaweza kuzivutia Simba, Yanga na Azam.