Bekele ajitoa London Marathon

LONDON, ENGLAND. MWANARIADHA wa Ethiopia, Kenenisa Bekele hatoshindana tena na mpinzani wake raia wa Kenya,  Eliud Kipchoge kwenye mbio za  London Marathon kutokana na Muithiopia huyo kupata majeraha ya misuli ya kigimbi.

Bekele, 38, alikuwa na sekunde mbili tu pungufu ya Kipchoge ambaye aliweka rekodi ya ulimwengu wakati akishinda Mashindano ya Berlin Marathon mwaka jana ya kukimbia kwa saa 2:01:39.

"Nimevunjika moyo sana," anasema Bekele.

"Nilifunga mguu wangu wa kushoto lakini baada ya kufanya mazoezi mambo yakawa tofauti. Niliamini kwamba nitakuwa tayari.

Ameongeza: "Mashindano haya yalikuwa muhimu sana kwangu. Kufanya kwangu vizuri Berlin mwaka jana ilinipa ujasiri mkubwa na motisha.

"Samahani kwa kuwakatisha tamaa mashabiki wangu, waandaaji na washindani wenzangu."

Kufuatia kujitoa kwa Bekele kutokana na kusumbuliwa na majeraha ni wazi kuwa kwa sasa Kipchoge wa Kenya ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kushinda mbio hizo za London Marathon.