Bayern yakubali yaishe kwa Thiego

Muktasari:

KOCHA wa Bayern Munich, Hansi Flick amesema kwamba anaelewa kwanini kiungo wa Kihispaniola, Thiago Alcantara, anayesakwa na Liverpool anataka kwenda kukipiga kwenye Ligi Kuu England.

MUNICH, UJERUMANI

KOCHA wa Bayern Munich, Hansi Flick amesema kwamba anaelewa kwanini kiungo wa Kihispaniola, Thiago Alcantara, anayesakwa na Liverpool anataka kwenda kukipiga kwenye Ligi Kuu England.

Mwenyekiti wa klabu hiyo mabingwa wa Bundesliga, Karl-Heinz Rummenigge alithibitisha wiki iliyopita kwamba Thiago anataka kuondoka, aende akapambane na changamoto mpya kwingineko.

Liverpool wanapewa nafasi kubwa ya kunasa huduma ya staa huyo wa kimataifa wa Hispania, licha ya mabingwa wa Ligue 1, Paris Saint-Germain nao wanahitaji saini ya mchezaji huyo anayethaminishwa kuwa na thamani ya Pauni 36 milioni.

Akiwa amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake, Flick amekubaliana na hali halisi juu ya kumpoteza staa huyo ndani ya wiki chache zijazo, huku Ligi Kuu England ndiyo inayotajwa kwamba atakwenda.

“Naelewa wakati mchezaji anapotaka kuondoka,” alisema.

“Thiago aliichezea FC Barcelona ya Hispania na FC Bayern Munchen ya Ujerumani. Kama anataka kwenda Ligi Kuu England kwa sasa, mimi namwelewa sana. Lakini, ni bahati mbaya sana, kwa sababu amekuwa akitufanyia mambo mazuri. Ukweli ningependa abaki kwa miaka michache ijayo, lakini haya ni maisha, lazima yaendelee.”

Thiago alicheza aliichezea Bayern Munich mechi 36 katika michuano yote msimu huu na leo Jumamosi atakuwa na majukumu ya kuitumikia timu yake kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya watakapokipiga na Chelsea.