Bayern yajifua kwa mafungu

Muktasari:

Timu za Ligi Kuu Ujeruman, zimeanza mazoezi kwa tahadhari kipindi hiki ambacho kuna janga la corona ili kujiandaa na mikiki ya Ligi Kuu nchini humo ambayo inatarajiwa kurejea mwishoni mwa mwezi huu.

Munich, Ujeruman. Miamba ya soka la Ujeruman, Bayern Munich ni miongoni mwa klabu za Ligi Kuu nchini humo maarufu kama Bundesliga ambazo zimeanza mazoezi kwa mara ya kwanza tangu kusitishwa kwa ligi hiyo.
Bundesliga ilisitishwa kama ilivyo kwa ligi nyingine kubwa barani Ulaya ikiwa ni hatua ambazo zilichukuliwa za kuzuia kusambaa zaidi kwa virusi vya corona.
Mabingwa hao, walionekana kufanya mazoezi katika makundi ya wachezaji watano watano bila ya kugusana kama ambavyo walionekana kufanya wachezaji wa Borussia Monchengladbach na  Wolfsburg katika program zao.
Paderborn ambao wapo kwenye hatari ya kushuka daraja katika mazoezi yao walionekana kuwa makini nao kama ilivyo kwa wenzao huku kocha wao, Steffen Baumgart akisema ni muhimu wachezaji kuendelea kuwa katika viwango vyao, "Wanatakiwa kuwa fiti."
Ligi za madaraja tofauti  nchini Ujeruman zilisitishwa tangu Machi 13 hadi Aprili 30 na itategemea na hali itakavyokuwa, kama ikiwa shwari basi huenda mikiki ya Ligi hizo ikaendelea.
"Yamekuwa mazoezi tofauti ni vile ambavyo imezoeleka katika makundi ambayo yalikuwa na uangalizi wa hali ya juu, nimefurahi kuonana na wachezaji wenzangu kwa mara nyingine tena," alisema nahodha wa Bayern, Manuel Neuer.
Bayern  wapo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Ujeruamn wakiwa na pointi nne zaidi ya  Borussia Dortmund ambao wapo nafasi ya pili