Bayern wameanza kuteseka huko!

Muktasari:

Straika fundi wa mabao wa klabu hiyo, Robert Lewandowski ameponda sera za usajili akisema wameondoka wachezaji wakubwa watatu lakini hakuna jambo lililofanyika.

Munich, Ujerumani. UFALME wa Bayern Munich umeanza kuingia doa huko Bundesliga na sasa wameanza kulaumiana tu.

Kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Borrusia Dortmund kwenye Super Cup kimewatia hofu kwamba, huenda ukawa mwisho wa ubabe wao.

Bosi wa Bayern Munich, Karl-Heinz Rummenigge aliondoka uwanjani baada ya mchezo huo akiwa amefura kwa hasira huku wachezaji wakiishia kurushiana lawama.

Straika fundi wa mabao wa klabu hiyo, Robert Lewandowski ameponda sera za usajili akisema wameondoka wachezaji wakubwa watatu lakini hakuna jambo lililofanyika.

“Nadhani tunahitaji wachezaji wakubwa watatu wapya, tumewapoteza washambuliaji watatu wakali (Franck Ribery, Arjen Robben na James Rodriguez), lakini mpaka sasa hakuna usajili mpya katika maeneo hayo,” alisema Lewandowski.

Kwa muda mrefu Bayern wamekuwa wakitamba kwenye soka la Ujerumani huku wakibeba wachezaji wa maana wakati wa dirisha la usajili, lakini msimu huu wamekuwa kimya.

Awali, Kocha wa Bayern Munich, Niko Kovac alikuwa kwenye rada za kuwanasa kinda wa Kiingereza, Callum Hudson-Odoi kutoka Chelsea, lakini dili hilo limekwama kutokana na kutakiwa kuvunja benki.

Pia, walifukuzia huduma ya kinda wa Manchester City, Leroy Sane lakini majeruhi aliyoyapata kwenye mechi za maandalizi ya msimu yakawarudisha nyuma.

Hata hivyo, Bayern mapema jana wametangaza kumnasa winga wa Inter Milan, Ivan Perisci, ambaye atakwenda kuwa mbadala wa Arjen Robben.

WALINASWA

Fiete Arp (Hamburg, £2.7m), Lucas Hernandez (Atletico Madrid, £68m), Benjamin Pavard (VfB Stuttgart, £31m)

WALIOTOKA

Frank Evina (KFC Uerdingen), Adrian Fein (Hamburg), Marco Friedl (Werder Bremen), Mats Hummels (Borussia Dortmund), Wooyeong Jeong (Freiburg), Rafinha (Flamengo), James Rodriguez (Real Madrid), Franck Ribery na Arjen Robben.