Basata kukagua nyimbo kwa ‘WhatsApp’

Muktasari:

Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), limeanzisha utaratibu wa kukagua nyimbo za wasanii kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp, jambo linaloelezwa kumuondolea usumbufu msanii kwenda ofisi za Basata.

Dar es Salaam. Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), limeanzisha utaratibu wa kukagua nyimbo za wasanii kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp.

Akizungumza leo Oktoba 22, Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza, amesema wamefikia hatua hiyo kama njia ya kuwarahisishia wasanii kukaguliwa kazi zao.

Sababu nyingine amesema ni kutokana na kukua kwa teknolojia wameona nao waendane sambamba na ulimwengu huo.

Mngereza alizitaja namba hizo kuwa ni 0783 965 337, ambapo msanii atatuma kazi yake na kupewa majibu haraka kama inafaa kwenda kwa jamii au la.

“Teknolojia imekuwa kubwa sana, hatuoni tena sababu ya kumsumbua msanii aje ofisi kwetu kwa ajili ya kukaguliwa nyimbo wakati kazi hiyo anaweza kuifanya hata akiwa nyumbani kwake.

“Pia, tunaamini itampunguzia gharama na kuokoa muda ambao atautumia kufanya mambo mengine, hivyo wale waliokuwa na visingizio ya hayo sasa hatufikirii tena kuvisikia kwani tumewarahisishia maisha ni wao wenyewe,” amesema Mngereza.

Akizungumzia hali ya wasanii kupeleka kazi zao kukaguliwa kabla ya kuzitoa, alisema kwa sasa uelewa umeongezeka kwa baadhi yao ambapo kwa siku wanaweza kupata hadi kazi 15 zinazotakiwa kukaguliwa.

Amesema anaamini kwa kutumia WhatsApp utaratibu ambao wameuanzisha mwezi mmoja uliopita utasaidia kuongeza mwitikio.

Ikumbukwe Februari mwaka huu, Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) ilizifungia nyimbo 15 za wasanii kadhaa zikiwemo mbili za Diamond kutokana na kuwa na maudhui ambayo yanaenda kinyume na maadili na kanuni za Huduma za Utangazaji (Maudhui) 2005.

Pia katika katazo hilo, TCRA iliviagiza vituo vya redio na vituo vya TV visitishe kuonesha na kuzicheza nyimbo hizo.

Nyimbo hizo na jina la msanii aliyeimba  kwenye mabano ni  Hallelujah na Wakawaka (Diamond), Kibamia (Roma Mkatoliki), Pale Kati patamu, Maku (Makuzi) na Mikono Juu (Ney wa Mitego), Hainaga Ushemeji (Manifongo), I am Sorry JK (Nikki Mbishi).

Nyingine ni Chura (Snura) na Nimevurugwa (Snura), Tema mate tumchape (Madee), Uzuri wako (Jux), Nampa papa (Gigy Money), Nampaga (Baranaba) na Bongo Bahati mbaya (Young D).