Barnabas apewa kazi ya Katwila

Morogoro. Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila ameachana na miamba hiyo na kutimkia Ihefu FC ya Mbarali, Mbeya.

Taarifa zilieleza kuwa Mtibwa Sugar inapanga kuziba nafasi yake kwa kumpa mikoba nyota wa wao wa zamani, Vicent Barnabas aliyekuwa akiinoa timu ya vijana.

Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru alisema amepata taarifa ambayo haikuwa rasmi kuwa kocha wao mkuu, Katwila amejiunga na Ihefu FC.

Kifaru alisema baada ya kutoka Mwanza walirudi na Katwila hadi kambini, lakini juzi alipokea taarifa ya kuondoka kwa Katwila.

“Kocha msaidizi, Barnabas aliniambia Katwila ameondoka na hakutokea katika mazoezi Jumamosi, baada ya kumtafuta aliniomba ruhusa kwenda nyumbani kwake kwa ajili ya kumaliza matatizo ya kifamilia,” alisema.

Mmoja wa wachezaji wa Ihefu, Emmanuel Kichiba, alikiri kumwona Katwila kambini kwao Mbeya.
“Sijui lolote kuhusu Katwila, lakini nimemuona hapa kambini kwetu,” alisema Kichiba.

Katibu wa Ihefu, Athumani Mndolwa alisema wapo katika mazungumzo na makocha wawili mzawa mmoja na wa kigeni.