Barnaba, Bella ndani ya Miss Moro

Muktasari:

Akifafanua juu ya mtazamo wa wadau kuona mashindano ya urembo ni kama uhuni ambapo baadhi ya wazazi huwakataza watoto wao kushiriki mmoja wa wanakamati aliyewahi kutwaa taji hilo, Doroth Mwatenga alisema hiyo ni dhana potofu.

WAREMBO12 kutoka pande mbalimbali za Mkoa hapa wanatarajiwa kupanda jukwaani kuwania taji la Miss Morogoro 2019 kesho Jumamosi huku burudani zikitarajiwa kutolewa na na wanamuziki Christian Bella na Barnabas.
Mratibu wa shindano hilo, Farida Fujo amesema wameandaa donge nono la fedha kwa mshindi tofauti na miaka iliyopita ambapo mara nyingi hupewa zawadi ya gari.
"Tofauti na miaka mingine safari hii tumeandaa fedha taslimu kwa mshindi, tumezingatia maelekezo ya Kamati ya Miss Tanzania kuwa tusitoe gari kutokana na sababu mbalimbali kwani gari litatolewa kwenye mashindano ya kitaifa pekee, hivyo kutoa fedha taslimu sio kama tumefulia, tumejiandaa vya kutosha, kiwango hicho tutakitangaza baadaye,"alisisitiza Farida.
Akifafanua juu ya mtazamo wa wadau kuona mashindano ya urembo ni kama uhuni ambapo baadhi ya wazazi huwakataza watoto wao kushiriki mmoja wa wanakamati aliyewahi kutwaa taji hilo, Doroth Mwatenga alisema hiyo ni dhana potofu.
"Na zaidi ndio maana sisi kama wanawake  tukaamua kuandaa shindano hili kwa mwaka wa pili sasa ili kufuta hiyo dhana iliyokuwepo, mashindano ya urembo ni sawa na michezo mingine na fursa ya kuibua vipaji na ajira, wazazi wasikatishwe tamaa, wawaruhusu watoto wao kushiriki mashindano haya," alisema Doroth
Akasema warembo watakaochuana kuwania taji hilo wako vizuri kuipeperusha Morogoro kitaifa na bendera ya nchi kimataifa na kwamba kila mrembo ana sifa za ziada hali inayotarajiwa kuwapa wakati mgumu majaji kumchagua yule atakayewakilisha Mkoa wa Morogoro.
Msemaji wa Kamati ya Miss Morogoro 2019, Warda Makongwa, amesema wasanii  mbalimbali wa ndani na nje ya mkoa huu wanatarajiwa kupamba onesho hilo akiwemo Barnabas na Christian Bella.
"Mtu asithubutu kukosa, kwani maandalizi yaliyofanyika ni kabambe na yanaridhisha, Jumamosi sio mbali, viingilio ni rafiki kwa kuanzia Sh 10 na kuendelea kwa kulenga makundi yote ya kijamii kutoikosa nafasi hii"alisisitiza Warda.