Bares abeti kwa Simba

Saturday January 12 2019

 

By Mwanahiba Richard

KOCHA wa zamani wa Tanzania Prisons, Mohamed Abdallah 'Bares' na mama yake mzazi Hafsa Mohamed Othman wameiambia Simba lazima ishinde ili iweke heshima kwa Watanzania na Afrika kwa jumla.
Simba leo Jumamosi ina kibarua cha kucheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mama mzazi na Kocha Bares, ambaye yeye ni Yanga lialia amesema hana mapenzi na Simba, lakini kwa kuwa inawakilisha nchi ni lazima aiombee mema na ifunge mabao mengi.
"Mechi ikiisha tu narudi kwangu Yanga, hao nawasapoti kwa muda tu na si vinginevyo, Simba washinde tena wapate magoli mengi tu hapa nyumbani naamini wanaweza na tunapaswa kuwa wazalendo sasa.
"Huwa naumia sana Yanga inapofungwa kwa ukweli inakuwa tafrani kwenye moyo wangu hata walipofungwa na kuondolewa kwenye mashindano ya Mapinduzi niliumia ila, ndio hakuna namna kwa kuwa kila kitu kina mipango," alisema Hafsa
Kwa upande wa Bares alisema "Huu ni wakati wa Simba kukumbushia enzi zao ambapo walifanya vizuri kwenye michuano kama hii. Hata safari hii wanaweza kwani wana kikosi kizuri sana na kipana, kocha ana uwezo wa kuamua jinsi gani awatumie wachezaji wake.
"Naitakia mafanikio Simba katika michuano hii na hata wachezaji wao wajitambue nini Simba inataka kipindi hiki," alisema Bares.

Advertisement