Bares: Ligi ngumu ila tutaboa tu

Muktasari:

Timu hiyo iko nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi baada kushinda michezo minne na kutoka sare michezo mitatu huku ikiwa na pointi 15

BAADA ya kupokea kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Yanga jana, kocha wa JKT Tanzania, Abdallah Mohammed 'Bares' amekiri ligi imekuwa ngumu lakini anaamini bado wana nafasi ya kufanya vizuri zaidi katika michezo yao ijayo.

Huo unakuwa mchezo wa nne JKT Tanzania kupoteza  katika michezo 11 waliyocheza hadi sasa tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Timu hiyo iko nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi baada kushinda michezo minne na kutoka sare michezo mitatu huku ikiwa na pointi 15

Bares amesema kadri ligi inavyochanganya kila timu inaimarika hivyo kusababisha mechi nyingi kuwa ngumu kwani hakuna timu inayokubali kufungwa kizembe.

"Tumepoteza mchezo hivyo hatuna budi kukubali na kuganga yajayo. Ligi imekuwa ngumu kwani kila timu kwa sasa imejiandaa.

"Kila timu ina mzunguko wa matokeo tofauti na mwanzo, yaani unaweza kwenda ugenini  ukashinda na ukacheza nyumbani ukapoteza na hali hiyo inaonyesha jinsi timu nyingi kwa sasa zilivyo vizuri.
 
"Kila siku zinavyoenda timu zinapata maandalizi ya kutosha  hivyo zinazidisha ugumu wa ligi tofauti na mwanzoni mwa msimu ambapo timu nyingi hazikuwa na maandalizi mazuri na nyingi ziliathiriwa na ukata"alisema Bares

Bares alisema wataendelea kupambana kuhakikisha msimu huu wanamaliza nafasi nne za juu pasipo kuangalia matokeo yaliyopita.