Barcelona yamtaka Moreno wa Liverpool

Muktasari:

Barcelona ilimuuza mlinzi wake wa kushoto Lucas Digne kwenda Everton, inahaha kumsaka mrithi wake na ipo tayari kutoa kiasi chochote kumsajili Alberto Moreno wa Liverpool.

Barcelona, Hispania. Barcelona inajiandaa kuwasilisha ofa mpya kwa Liverpool kwa lengo la kumsajili beki Alberto Moreno.
Kocha Ernesto Valverde anaamini safu ya ulinzi ya Barcelona bado inayumba ndio maana timu hiyo imeshindwa kufanya vema katika mechi zake za hivi karibuni na Moreno itakuwa suluhisho.
Moreno amekuwa chaguo la kwanza la Liverpool katika beki ya kushoto tangu kutua kwa Kocha Jurgen Klopp na mchezaji huyo aliyesajiliwa mwaka 2014 kutoka Sevilla kwa sasa anajiandaa kusaini mkataba mpya.
Mchezaji huyo amecheza mechi 88 na kufunga mabao matatu na mwanzoni kulikuwa na wasiwasi kwamba angepoteza namba kwa mchezaji mpya Andy Robertson aliyetua Anfield mwaka 2017, lakini mambo yamekuwa tofauti.
Haijajulikana iwapo Moreno atakubali kwenda Barcelona na kuwa chaguo la pili kwani chaguo la kwanza ndani ya timu hiyo ni Jordi Alba ambaye kwa sasa amepona majeraha yaliyomuweka nje kwa kipindi kirefu.
Barcelona inajutia uamuzi wa kumuuza aliyekuwa mlinzi wake Lucas Digne ambaye alienda Everton kwa Pauni 20, milioni katika siku ya mwisho ya dirisha la usajili wa kiangazi Agosti mwaka huu.
Mbali ya mlinzi huyo Barcelona pia inamsaka kiungo chipukizi wa Paris Saint Germany, Adrien Rabiot, ingawa timu yake inataka dau kubwa la Pauni 133 milioni ili kumuachia.