Barcelona yagonga mwamba kwa Neymar

Wednesday August 14 2019

 

Madrid, Hispania. Jaribio la Barcelona kumrejesha katika kikosi chake nyota wa zamani Neymar zimegonga mwamba.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Barcelona, Eric Abidal, alikwenda Paris Saint Germain (PSG), kumalizana na klabu hiyio, lakini alikwaa kisiki.

Barcelona iliweka mezani Pauni74 milioni na kumtoa kwa mkopo Phillip Coutinho, lakini zilikataliwa na mabingwa wa Ligi Kuu Ufaransa.

PSG inataka zaidi ya fedha hizo na wachezaji wengine kumtoa Neymar kabla ya dirisha la usajili kufungwa Septemba 2.

Wiki iliyopita wakala wa Neymar, Pini Zahavi alizungumza na Real Madrid kuhusu uhamisho wa mteja wake lakini mpango huo ulikwaa kisiki.

Rais wa Barcelona Josep Bartomeu alimuagiza Abidal, Javier Bordas na Andre Cury kwenda kuzungumza na Mkurugenzi wa Ufundi wa PSG Leonardo na msaidizi wake Angelo Castellazzi.

Advertisement

Hata hivyo baada ya kikao cha vigogo hao, PSG ilitaka nyongeza ya dau la ofa na kuongeza wachezaji wengine badala ya Coutinho.

Huenda Barcelona ikamuongeza Ivan Rakitic ili kukamilisha mpango wa kumrejesha Neymar.

PSG inataka jumla ya Pauni206 ili kulinganisha na thamani ya nahodha huyo wa zamani Brazil.

Advertisement