Barcelona yaanza kupotezwa La Liga

Monday October 8 2018

 

Madrid, Hispania. Bingwa mtetezi wa Ligi Kuu ya Hispania, Barcelona, imestushwa na kiwango chake duni msimu huu baada ya juzi kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Valencia, ikiwa ni ya nne mfululizo katika ligi hiyo.

Sare hiyo imeifanya Barcelona kung’olewa kileleni na sasa ipo nafasi ya pili, ikiwa moja nyuma ya vinara Sevilla yenye pointi 16 zote zikiwa zimecheza mechi nane.

Kosa lililofanywa na mlinzi Gerard Pique katika dakika ya nne ya mchezo aliyepiga fyongo liliigharimu timu hiyo kwani Ezequiel Garay alilitumia kuipatia Valencia bao la kuongoza, kabla ya Lionel Messi kusawazisha dakika ya 23.

Bao hilo la Messi limemfanya kuwa mchezaji anayeongoza kwa kuifunga na kutoa pasi za mabao nyingi zaidi dhidi ya timu hiyo katika La Liga akiwa amefunga mabao 22 na kutoa pasi 10 zilizoza mabao.

Matokeo hayo yameifanya Barcelona kutoshinda katika mchezo wan ne mfululizo katika La Liga, ikiwa ni mara ya kwanza kwao kwa zaidi ya misimu mitatu.

Barcelona walimiliki mpira kwa asilimia 75 lakini wakakosa mbinu za kufunga kutokana na wenyeji kuamua kupaki basi, hivyo matokeo kuifanya Sevilla iliyoishinda Celta Vigo kwa mabao 2-1 kupanda hadi kileleni.

Baada ya mchezo huo Kocha wa Barcelona, Ernesto Valverde, alielezea kusikitishwa na kinachotokea lakini akawatetea wachezaji wake akisema uchovu ndio unaowagharimu.

“Naamini kinachoiangusha Barcelona kwa sasa ni kukamiwa zaidi na kila timu, huku pia wapinzani wakicheza kujilinda kwa muda wote wa mchezo jambo linalowapa kazi pevu kufunga huku wakilazimika kucheza kwa kutumia nguvu nyingi katika kila mchezo,” alisema Valverde.

Katikati ya wiki iliyopita Barcelona ilionyesha mchezo mzuri na kuibuka na ushindi dhidi Tottenham mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliochezwa ugenini.

Advertisement