Barca warudi tena kwa Griezmann

Muktasari:

  • Kwenye mkataba wa Griezmann imeripotiwa kuwapo na kipengele kinachohitaji kulipiwa Pauni 120 milioni kwa timu itakayohitaji kunasa saini ya mchezaji huyo na Barcelona inaweza kutoa pesa hiyo kwa sababu mwishoni mwa msimu itaingia sokoni kusaka mrithi wa Luis Suarez.

BARCELONA, HISPANIA.BARCELONA imekuja na mpango wa kuzindua upya mkakati wake wa kumnasa fowadi wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann.

Ripoti zinadai vinara hao wa La Liga wameamua kumweka tena kwenye rada zao Mfaransa huyo baada ya kushindwa kuinasa huduma yake kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Kwenye usajili wa majira ya kiangazi mwaka jana, Griezmann alitajwa sana angekwenda kutua Nou Camp kabla ya jambo hilo kukwama na supastaa huyo wa Les Bleus kuamua kusaini mkataba mpya wa kuendelea kukipiga Atletico Madrid.

Wakati ikionekana dili hilo lisingetokea tena, Gazeti la Ufaransa la L’Equipe linafichua Barcelona haijafuta dhamira na nio yake ya kumnasa staa huyo matata kabisa.

Kwenye mkataba wa Griezmann imeripotiwa kuwapo na kipengele kinachohitaji kulipiwa Pauni 120 milioni kwa timu itakayohitaji kunasa saini ya mchezaji huyo na Barcelona inaweza kutoa pesa hiyo kwa sababu mwishoni mwa msimu itaingia sokoni kusaka mrithi wa Luis Suarez.

Griezmann, ambaye aliwahi kuichezea Real Sociedad amefunga mabao 91 kwenye ligi katika kipindi chake chote alichodumu katika mji huo mkuu wa Hispania, Madrid.