Barca wamzidi ujanja Lampard kwa straika wa kibabe

Muktasari:

Taarifa za kutoka huko Hispania zinadai fowadi huyo wa Inter Milan ameshafikia makubaliano binafsi na Barcelona kwa ajili ya kujiunga nao dirisha lijalo majira ya kiangazi.

BARCELONA, HISPANIA . FRANK Lampard ana Pauni 300 milioni zake mkononi kwa ajili ya kufanya matumizi ya kusajili kukifuma kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao.

Lakini, wanoko wala hawakujali kama ana pesa ndefu hivyo, walichokifanya ni kuvamia mawindo yake na kufanya mambo.

Barcelona buana, wanadaiwa kumpiga za uso Lampard na chama lake la Chelsea kwenye mbio za kumsajili fowadi hatari wa Kiargentina, Lautaro Martinez.

Taarifa za kutoka huko Hispania zinadai fowadi huyo wa Inter Milan ameshafikia makubaliano binafsi na Barcelona kwa ajili ya kujiunga nao dirisha lijalo majira ya kiangazi.

Kocha Lampard alikuwa amemweka Martinez kwenye orodha ya washambuliaji anaowataka akakipige Stamford Bridge msimu ujao na kwa kupewa Pauni 300 milioni aliona jambo hilo wala lisingekuwa tatizo, angeweza kuwapa kiasi chochote cha pesa Inter ili kunasa saini ya mchezaji huyo.

Lampard anataka kuleta straika mpya kwenye kikosi chake cha The Blues ili kwenda kusaidiana na Tammy Abraham kwenye fowadi baada ya Olivier Giroud kuelekea mlango wa kutokea kwenye kikosi hicho.

Lakini, kuhusu Martinez, 22, saini yake imekuwa na upinzani mkali na staa huyo inadaiwa kufikia makubaliano na Barca kwenye mambo binafsi na anachosubiri ni timu hizo mbili kufikia makubaliano kufunga biashara.

Kwenye dili hilo, kitu kinachowavuruga Inter Milan ni kipengele chao cha kutaka kulipwa Pauni 100 milioni walichokiweka kwenye mkataba wa mshambuliaji huyo kinaweza kusiwe na maana yoyote na kujikuta wakikosa mkwanja huo.

Miamba hiyo ya Serie A, imeweka kipengele kinachoelekeza kama kuna timu inamtaka Martinez basi wanapaswa kulipa Pauni 100 milioni, lakini hiyo ni kama atasajiliwa kati ya Julai Mosi hadi Julai 15. Huo ndio muda ambao Inter walipanga kumuuza mshambuliaji huyo kinyume cha hapo, basi isingefanya biashara.

Lakini, kutokana na janga la virusi vya corono vilivyofanya msimu kusimama na bila ya shaka hata dirisha la usajili litachelewa kufunguliwa, jambo linafanya kipengele hicho alichokiweka kwenye mkataba kutokuwa na thamani tena.

Wakati huo, wale wachezaji wote ambao mikataba yao ilikuwa ikimalizika Juni 30 watalazimika kubaki kwenye timu zao hadi msimu utakapomalizika kwa mujibu wa taarifa ya Fifa. Barca wao licha ya kutofahamu hatima ya msimu huu utakavyomalizika, wameona ni wakati wa kufanya kweli kwenye kuweka mipango sawa ya kukamilisha usajili wa wachezaji wanaowataka.

Wanaripotiwa kuwasiliana na Martinez na kukubaliana mambo binafsi. Taarifa zinasema ilikuwa ngumu kwa Martinez kugomea nafasi ya kwenda kucheza na Muargentina mwenzake Nou Camp, Lionel Messi.

Inter wao kwa sasa wanafanya mipango ya kuhakikisha wanavuna zaidi ya Pauni 100 milioni kwenye mauzo ya mchezaji huyo. Martinez amefunga mabao 19 katika mechi 32 za michuano yote aliyocheza msimu huu kwa klabu na timu yake ya taifa.

Barca sasa wanasubiri kwenda kuzungumza na mabosi wa Inter wakiamini watawashawishi kumsajili kwa ada ndogo huku wakipanga kuwatumia mastaa kadhaa kukamilisha dili hilo.

Taarifa za mapema wiki hii za kutoka Italia zinadai Barcelona imewaweka ubaoni wachezaji wake watano kwenye kikosi cha kwanza kwa ajili ya kuwalainisha wakali hao wa Serie A ili kumwaachia mshambuliaji wao huyo kwa kupewa pesa pamoja na mchezaji mmoja kwenye orodha hiyo y wakali watano.

Miongoni mwa wachezaji hao ni kiungo Arturo Vidal, ambaye aliwindwa sana na Inter Milan kwenye dirisha la usajili wa Januari. Kiungo wa Kibrazili, Philippe Coutinho, ambaye yupo kwa mkopo kwa sasa huko Bayern Munich, naye ameambiwa nyakati zake zimefika mwisho huko Nou Camp na bila shaka atakuwa kwenye orodha ya wachezaji hao watano ambao Barca imepanga kuwatumia kunasa wachezaji inaowasaka.