Barca wainyatia Madrid kwenye mbio za ubingwa

Muktasari:

Barca baada ya kushinda imepunguza pengo la alama kati yake na Madrid ambayo ipo kileleni kwa tofauti ya pointi moja, Madrid ikiwa na 77 na Barca 76. Lakini Madrid wana faida ya mchezo mmoja mkononi.

BARCELONA, HISPANIA. LIGI Kuu Hispania imeendelea hapo jana kwa michezo minne kupigwa, ambapo pale kunako dimba la Camp Nou, Barcelona ikazidi kuwatikisa Real Madrid kwenye mbio za ubingwa baada ya kupata ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Espanyol.

Barca baada ya kushinda mecho hiyo imepunguza pengo la alama kati yake na Madrid ambayo ipo kileleni ambapo hivi sasa wana tofauti ya pointi moja, Madrid ikiwa na 77 na Barca 76. Lakini Madrid wana faida ya mchezo mmoja mkononi.

Baada ya mchezo huo, kocha wa Barcelona Quique Setien alikiri kuwa timu yake haikucheza vizuri, licha ya kuibuka na ushindi,

"Hatukucheza vizuri leo, Espanyol walifunga mianya yote na ilikuwa ngumu kuwafungua na kuwafunga, kiukweli ilikuwa ni mechi ngumu"alisema.

"Tunafanya kile ambacho tunapaswa kufanya na sio kingine bali ni ushindi, kwa sasa tunawaangalia Madrid, kwani chochote kinaweza kutokea ndani ya ligi, nafahamu kuwa hatukucheza vizuri kama tulivyocheza na Villarreal, lakini tulijaribu kufanya kila kitu lakini Espanyol walionekana kuwa bora sana kwenye kutuzuia' aliongeza.

Bao pekee na la ushindi kwa Barca lilifungwa na Luis Suarez dakika ya 56, lakini kinda wao Ansu Fati alipata kadi nyekundu dakika ya 50, huku Kiungo wa Espanyol Pol Lozano, na yeye akipata kadi nyekundu dakika ya 56.

Michezo mengine miwili, ilikuwa ni kati ya Getafe dhidi ya Villarreal, ambapo Villarreal ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1. Lakini pia Real Betis ilimcharaza Osasuna mabao 3-0.