Barca, Madrid kuwanyemelea Mane na Salah

Muktasari:

Liverpool walitwaa ubingwa wa Ulaya wikiendi iliyopita huku wakiukosa kidogo ubingwa wa England msimu uliosha na Mane na Salah wamekuwa na mchango mkubwa kikosini hapo huku wakitengeneza moja kati ya safu bora ya ushambuliaji Ulaya.

LONDON, ENGLAND.HOFU imeanza kutanda kwa watu wa Liverpool. Tahadhari imetolewa na mtu mmoja anayejua fitina za soka. Anaamini kwamba mastaa wao wawili, Sadio Mane na Mohamed Salah lazima watafuatwa na klabu mbili kongwe za Hispania, Barcelona na Real Madrid.

Graeme Souness, staa wa zamani wa Liverpool ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka ana hofu kwamba huenda yale yaliyotokea kwa Luis Suarez na Philippe Coutinho yakajirudia kwa Sadio Mane na Mohamed Salah.

Liverpool walitwaa ubingwa wa Ulaya wikiendi iliyopita huku wakiukosa kidogo ubingwa wa England msimu uliosha na Mane na Salah wamekuwa na mchango mkubwa kikosini hapo huku wakitengeneza moja kati ya safu bora ya ushambuliaji Ulaya.

“Real Madrid na Barcelona watakuwa wananusanusa kuhusu Salah na Mane na nadhani mmoja kati yao lazima atawindwa katika dirisha hili la uhamisho. Timu zote hizo mbili zipo katika mchakato wa kujijenga upya na wana uwezo wa kumnyemelea mchezaji yeyote wanayemtaka” alisema Souness.

“Liverpool ni timu kubwa ya soka na wamethibitisha ubora wao kwa kurudi tena katika fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya pili mfululizo, lakini wachezaji wengi wanapata shida kusema hapana pindi Real Madrid na Barcelona zinapowafuata.”

“Tuliona hapo nyuma kwa Luis Suarez na Philippe Coutinho. Ingawa walikuwa wanafurahia kucheza soka Liverpool, lakini mawazo yao yalibadilika pindi walipotakiwa na Barcelona. Hilo litatokea tena kwa Mane na Salah,” aliongeza Souness.

Hata hivyo, Souness alikiri kwamba kwa sasa Liverpool wapo katika nafasi nzuri baada ya kutwaa taji la sita la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya Jumamosi iliyopita baada ya kuichapa Tottenham mabao 2-0 katika dimba la Wanda Metropolitano jijini Madrid.

Lakini anaamini kwamba Liverpool inabidi iwe na wasiwasi zaidi kuhusu wachezaji wanaoweza kuondoka kuliko wale wanaoweza kuingia huku pia akiwa na wasiwasi na nguvu ya matumizi ya pesa kutoka kwa wapinzani wao wakubwa katika Ligi.

“Liverpool wapo vizuri kwa miaka michache ijayo. Unamtazama golikipa, walinzi wanne, Joel Matip au Joe Gomez, safu yao ya ulinzi inaweza kucheza pamoja kwa miaka nane au kumi ijayo kama wakiepuka majeraha.” Alisema Souness.

“Trent Alexander-Arnold anaenda kuwa mchezaji mzuri zaidi, ana mguu wa kulia mwepesi. Andy Robertson anaweza kuwa pale kwa muda mrefu. Wanaweza kuongeza wachezaji katika kikosi walichonacho sasa kwa ajili ya kuimarisha, lakini kimsingi wana timu ambayo wanaweza kwenda nayo kwa miaka ming ijayo.”

“Wasiwasi wa Liverpool kwenda mbele siyo Manchester City kwamba wana nguvu za kutumia, bali ni namna ambavyo kuna timu inaweza kuja kwa Salah, kitu ambacho naamini watafanya, au Mane pia. Nadhani watakuwa katika orodha ya wachezaji wanaotakiwa Real Madrid. Liverpool wapo vema, sina wasiwasi na wao,” alisema. Kocha, Jurgen Klopp anatazamiwa kuimarisha kikosi chake licha ya kuwa bado hajaanza makeke ya usajili mpya.