Barbara: Meneja mpya Simba huyu hapa

Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez alikiri ni kweli wamewaondoa aliyekuwa Meneja Patrick Rweyemamu na Kocha wa Makipa, Muharami Mohamed na kusema tayari wameshampata mtu wa kuziba nafasi ya Rweyemamu kwa mapendekezo ya Kocha Sven.

“Nafasi ya Rweyemamu itashikiliwa kwa sasa na Ally Abbas Suleiman ambaye alikuwa mratibu wa timu, kwani anaonekana anafaa kwa sababu ya uzoefu alionao ndani ya timu,” alisema Barbara aliyesisitiza baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo ya mtendaji kumrithi Senzo Mazingisa amekuwa akirekebisha baadhi ya mambo ili kuifanya Simba iende kisasa.

Sio mara ya kwanza kwa Abbas kuwa meneja wa Simba, kwani alishawahi kuishikilia nafasi hiyo akipokezana na Nico Nyagawa miaka kadhaa iliyopita kabla ya kuteuliwa kuwa Mratibu wa timu, kitu kinachomfanya awe ni mzoefu kwenye benchi hilo la ufundi la Simba kulinganisha na wote waliopo sasa.