Bao la utata Simba lamng’oa mwamuzi

Muktasari:

Mwamuzi msaidizi Haji Mwarukuta ameondolewa katika orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kukataa bao linalodaiwa kuwa halali la Simba.

Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF Salum Chama, alisema Mwarukuta alishindwa kutafsiri vyema sheria ya kuotea hivyo ameondolewa katika orodha ya waamuzi.

Dar es Salaam. Bao lililokataliwa la kiungo mshambuliaji wa Simba, Mohammed Ibrahim dhidi ya Stand United juzi, limemponza mwamuzi msaidizi, Haji Mwarukuta kutoka Tanga ambaye ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi.
Mwarukuta alikataa bao hilo lililofungwa dakika ya 50 akidai Ibrahim aliotea kabla ya kufunga, baada ya kuwahi mpira uliogonga mwamba na kurudi uliotokana na shuti la faulo iliyopigwa na Said Ndemla, lakini kiuhalisia, kiungo huyo mshambuliaji wa Simba hakuwa ameotea.
Kukataliwa kwa bao hilo kumeibua mjadala miongoni mwa kundi kubwa la wadau wa soka ambao wengi wameshangazwa na uamuzi huo ambao uliinyima Simba nafasi ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0.
Simba ilishinda mabao 3-0, katika mchezo huo yaliyofungwa na Cletus Chama, Emmanuel Okwi na Meddei Kagere.
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) Salum Chama, aliliambia gazeti hili  wamemchukulia hatua mwamuzi huyo msaidizi kwa kushindwa kutafsiri sheria ya kuotea.
"Nadhani tatizo siyo TFF au Bodi ya Ligi  ni waamuzi wenyewe, ukiangalia lile bao wala haiitaji kazi ngumu kubaini lilikuwa ni halali lakini sijajua refa alifikiria nini hadi akakataa.
“Tumeshakutana kama kamati na kujiridhisha kuwa mwamuzi msaidizi alifanya makosa, hivyo tumemchukulia hatua kwa kumuondoa kwenye orodha ya waamuzi na tunatoa angalizo tutaendelea kuchukua hatua kwa waamuzi wote watakaochezesha chini ya kiwango," alionya Chama.
Akizungumzia bao hilo, aliyewahi kuwa  mwamuzi mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini, alisema kukataliwa kwa bao hilo kumetokana na uzembe binafsi wa  refa.
"Kanuni namba 11 inayozungumzia makosa ya kuotea, inafafanua wazi kwenye eneo la kuotea siyo kosa lakini hata hivyo pia mfungaji ukitazama marudio ya video, utaona kuwa wakati Ndemla anapiga lile shuti, hakuwa kwenye eneo la kuotea, shida kubwa inayowakabili waamuzi wengi wasaidizi ni kutomtazama mtu wa mwisho wakati timu inashambulia ndio maana zinatokea changamoto kama hizo," alisema mwamuzi huyo nguli nchini.
Kocha msaidizi wa Stand United, Athumani Bilali alisema ingawa mwamuzi hukosea kama binadamu wengine, ukataaji wa mabao halali unakatisha timu tamaa na kuwathiri wachezaji kisaikolojia.
"Unajua yapo mazingira ambayo mwamuzi akikosea unaweza kumsamehe lakini kukataa mabao halai huwa inaumiza. Kwa bahati mbaya makosa kama hayo yanaonekana timu hizo zinazoitwa kubwa zinapoathirika, lakini kiuhalisia sisi wenye timu hizi nyingine ndio tunaumia zaidi.
“Fikiria timu imetumia gharama kubwa kujiandaa, inacheza mpira mzuri lakini mtu mmoja tu anawanyima ushindi, inaumiza kwa kweli," alisema Bilali.
Kocha wa Prisons. Mohammed Abdallah 'Bares' alisema waamuzi hasa wa pembeni wanatakiwa kuwa makini kwa sababu wanasababisha kupatikana washindi wasiostahili.
"Nadhani sio uzembe wa waamuzi wote bali wachache tu ambao wanasababisha wengine waonekane pia hawafai. Kiukweli zinaathiri timu kwa kupoteza pointi lakini pia kisaikolojia kwa sababu timu moja inahukumiwa na kuumizwa pasipo kosa lolote.
Ilitokea kwenye mechi yetu dhidi ya Mbeya City ambapo tulifunga bao halali lililokataliwa sasa kwa ni vyema wakabadilika ili tupate washindi kwa haki.
Adhabu ya Mwarukuta kutoka Tanga, inamfanya kuwa mwamuzi wa tano kukutana na rungu la Kamati ya Waamuzi ya TFF kutokana na makosa ya kushindwa kutafsiri sheria 17 za soka.
Awali, waamuzi wanne waliondolewa kwenye orodha na kupewa adhabu ya kufungiwa vifungo vya muda tofauti ambao ni Jimmy Fanuel, Athumani Lazi, Nicholas Makaranga na Jamada Ahmada.